Italia yafikia deni la asilimia saba

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bw Silvio Berlusconi

Wakati waziri mkuu wa Italia Silvio Berlusconi akitangaza nia yake ya kujiuzulu mgogoro wa kiuchumi wa nchi hiyo umezidi kudhoofika.

Kutokana na mtafaruku wa kisiasa mjini Roma kiwango cha hisa ambacho Italia inatakiwa ilipe kwenye masoko ya hisa duniani kimepanda kwa asilimia saba.

Ni viwango kama hivyo ndivyo vilivyosababisha Ugiriki, Ireland na Ureno kuomba msaada.

Waziri Mkuu Berlusconi amesema atajiuzulu pindi atakapokamilisha msukumo wa mageuzi ya uchumi, ingawa bado kuna walakini juu ya serikali itakayofuata.

Hali kadhalika haijabainika kama utawala mpya utakuwa na nguvu ya kutuliza suala la fedha nchini humo.

Kuna wasiwasi kwamba hali hio imechagiza kupanda kwa kiwango cha riba ambayo Italia inalazimishwa kulipa kwenye masoko ya hisa.

Raia wa Italia wanafahamu kuwa nchi yao inazidi kudidimia kuelekea dimbwi hatari la kifedha na wapinzani wa Bw Berlusconi wanatoa hoja kwamba hizo ni sababu nyeti zinazofanya utawala mpya uwekwe mapema kuliko kusubiri.