Uzalishaji mafuta Sudan kusini wapungua

Haki miliki ya picha trevor
Image caption Sudan Kusini

Uzalishaji mafuta Sudan kusini umepungua kwa robo asilimia tangu kupata uhuru miezi minne iliyopita, waziri wa mazingira ameiambia BBC.

Tangu kujitenga na kaskazini kumekuwa na upungufu wa wafanyakazi wenye ujuzi, alisema William Garjang.

Alisema msimu wa mvua nao umesababisha ugumu wa kutengeneza mashine zilizoharibika na barabara tele zimechimbwa na waasi.

Mapato kutokana na mafuta hutoa asilimia 98 ya bajeti ya taifa hilo jipya.

Sudan kusini ilijitenga na Sudan mwezi Julai- baada ya kuwepo makubaliano mwaka 2005 iliyomaliza miongo ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Nchi hizo mbili bado hazijakubaliana namna ya kugawana utajiri huo wa mafuta.

Mwandishi wa BBC James Copnall huko Bentiu, mji mkuu wa jimbo la Unity, amesema kuna wasiwasi mkubwa kuhusu utegemezi mkubwa wa mafuta kwa Sudan kusini, hasa ukizingatia mafuta hayo yanaweza kuisha katika miongo miwili au mitatu ijayo.

Upinzani unaoendelezwa na kundi jipya la waasi, the South Sudan Liberation Army (SSLA), limeongeza matatizo kwenye suala hilo.

Wapiganaji wake wako zaidi jimbo la Unity, karibu na maeneo mengi ya mafuta yenye faida kubwa Sudan Kusini.

SSLA lilianza mapigano mapema mwaka huu kupinga ufisadi, ubadhirifu wa mapato ya mafuta na kwa kile wanachoamini ni kuwepo kwa wingi wa kabila la Dinka kwenye serikali.

Lakini Bw Garjang ameiambia BBC upinzani huo haukuwa unaingilia uzalishaji wa mafuta.

Alisema sehemu ya tatizo ni msimu wa mvua, uliosababisha ugumu katika kutengeneza mashine iliyokuwa imeharibika.

Lakini tatizo jengine kubwa ni kukosekana kwa wataalamu wa kiufundi, kwani wengi kutoka kaskazini waliondoka kwenye maeneo yenye visima vya mafuta baada ya Sudan kusini kupata uhuru, alisema Bw Garjang.