ILO yaonya kuhusu ukosefu wa ajira

Ripoti ya Shirika la Kazi la kimataifa, ILO, imeonya kuwa uchumi wa dunia uko ukingoni mwa hatua mpya na ya kuporomoka zaidi hali inayoweza kusababisha kukosekana kwa utulivu wa kijamii.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Misukosuko ya kijamii itatokea

ILO imebashiri kuwa ajira mpya milioni themanini zinahitajika katika miaka mitano ijayo ili kurejesha kiwango cha ajira cha kabla ya mdororo wa uchumi wa mwaka 2008, lakini limesema ni nusu tu ya ajira hizo zitakazopatikana.

Kulingana na utafiti wa shirika la kazi la kimataifa (ILO) kufuatia kuporomoka kwa uchumi duniani katika viwango vibaya zaidi itachukuwa zaidi ya miaka tano kubuni nafasi za kazi ambazo zinahitajika.

Shirika hilo linasema katika ya nchi 118 zilizofanyiwa utafiti 45 kati yazo zinakabiliwa na tishio la kuzuka kwa misukosuko ya kijamii kwa kuwa watu wengi hawana ajira.

Utafiti huo unaonyesha kuwa kwa sasa nafasi milioni 80 za kazi zinahitajika duniani ilikudhibiti hali. Lakini kutokana na hali mbaya ya uchumi ni nusu ya nafasi hizo zitakazo weza kupatikana.

Mwakilishi wa shirika hilo Raymond Torres ameiambia BBC kuwa imefikia wakati wa kujua mbivu na mbichi.

"Kumekuwepo na mjadala mrefu kuhusu kutatua tatizo la madeni na lile la usimamizi wa mfumo wa mashirika ya fedha, lakini hali ya ukosefu wa kazi umezidi kuwa mbaya. Kwa hivyo hili linatatiza na huenda asilimia 40 ya nchi zote duniani zikasuhudia misukosuko" amesema Bw Torres.

Kulingana na shirika hilo misukosuko hii huenda ikashuhudiwa sana uropa na katika nchi za kiarabu.

Na kwa upande wake shirika la maendeleo na ushirikiano wa kiuchumi, OECD limetaka viongozi wa nchini 20 tajiri duniani, G20 kufanya maamuzi ya kijasiri ambayo yatahakikisha usimamizi bora wa hazina za serikali.