Tovuti ya Madini yazinduliwa DRC

Joseph Haki miliki ya picha
Image caption Rais Kabila wa DRC aliingia madarakani 2006

Tovuti itakayotangaza kwa uwazi sekta ya madini katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambayo imegubikwa na mgogoro na rushwa imezinduliwa rasmi.

Shirika binafsi la Carter Center limesema limesaidia kuanzishwa tovuti ya congomines.org ili kuwapa watu wengi zaidi taarifa kuhusu sekta ya madini yakiwemo masuala ya mikataba na malipo.

Mamia ya nyaraka za madini na ramani zake zitakuwa ndani ya tovuti hiyo, limesema.

Jamhuri ya Kidemekrasi ya Congo ni nchi tajiri kwa dhahabu, almasi na coltan lakini migodi mingi inadhibitiwa na vikundi vyenye silaha.

Watu wa DRC ni miongoni mwa watu maskini zaidi barani Afrika ingawa nchi hiyo ni tajiri kwa raslimali.

Elizabeth Caesens, mkuu wa shirika hilo la Carter Center linachosimamia miradi ya madini nchini Congo alisema www.congomines.org itawarahisishia watu kufuatilia maendeleo ya sekta hiyo zikiwemo fedha zinazotengwa kwa maendeleo.

"Lengo letu kubwa ni kwa wakongo ambao wakati mwingine wanakosa taarifa kuhusu masuala ya kiufundi, uendeshaji wa migodi na mikataba, mapato na takwimu za uzalishaji”. Alisema Caesens.

Mwandishi wa BBC Thomas Hubert katika mji mkuu Kinshasa, anasema watu wengi wanaona sekta ya madini imegubikwa na usiri mkubwa hasa baada ya migodi inayomilikiwa na serikali kubadilishwa kwa mikataba ya siri na yenye utata.

Tovuti hiyo inajaribu kuwasaidia watu wazifikie kwa urahisi nyaraka –ziwe ni ripoti za serikali au takwimu za soko la Hisa la New York lenye orodha za makampuni yenye hisa zake katika migodi ya DRC, anaripoti mwandishi wa BBC.

Carter Center lililoanzishwa na Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter –limezindua tovuti hiyo kwa ufadhili wa serikali ya Belgium, koloni lake la zamani.

Mashariki mwa DRC kumekuwa na migogoro kwa karibu miaka 15 sasa huku wote jeshi na vikundi vya waasi vikituhumiwa kutumia mapigano kama kisingizio wakati vikichota utajiri wa madini katika eneo hilo.

Wachambuzi wanasema soko la kimataifa kwa madini ya Coltan ni mojawapo ya vyanzo vya mgogoro na kuwepo kwa wanamgambo nchini humo.

Mwezi Mei serikali iliondoa kizuizi kwenye machimbo ya mashariki, eneo lililoathiriwa zaidi na migogoro ya DRC ya muda mrefu.

Makampuni ya kigeni ndio wawekezaji wakubwa nchini DRC.