Waasi wa SPLM-kaskazini washambulia

Kwa mujibu wa jeshi la Sudan mamia ya waasi wameuawa katika jimbo la kusini mwa Sudan la Kordofan kufuatia mapambano na jeshi.Madai hayo hatahivyo yanapingwa na waasi.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Msemaji wa jeshi la Sudan Sawami Khaled Saad

Gavana Ahmed Haroun amesema kuwa waasi wa kaskazini wa SPLM waliuawa wakati, jeshi lilipokabiliana nao katika mji wa Toladi.

Lakini msemaji wa waasi amesema mapigano yaliendelea na wanajeshi wengi wa serikali waliuawa.

Talodi ni mji upo karibu na mpaka na Sudan Kusini, ambayo ilipata uhuru wake kutoka Sudan mwezi July.

Mwandishi wa BBC James Copnall akiwa mjini Khartoum anasema kuukamata mji wa Talodi itakua ni hatua kubwa ya ufanisi kwa waasi wa SPLM wa kaskazini.

Anasema kuwa wanadhibiti maeneo makubwa ya kusini mwa Kordofan, ingawa ni maeneo ambayo yanatatiza sana kuyafika kwa kuwa yako milimani.

Waasi hao pia wanakabiliana na serikali katika jimbo la Blue Nile, lakini mwandishi wetu anasema haya ni mapigano ambayo ni madogo sana kwa serikali.

"Mamia ya wapiganaji wa SPLM-kaskazini waliuawa wakati wa mashambulio katika mji wa Talodi mapema leo asubuhi" alisema Bw. Haroun.

Bw. Haroun anatakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC kwa shutuma za uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur, alikokuwa gavana, na mwandishi wetu anasema Haroun anaogopewa na waasi wa SPLM-kaskazini.

Makundi ya haki za binadamu yamelishutumu jeshi kwa kufanya mauwaji ya kimbari kusini mwa Kordofan dhidi ya watu wa Nuba wanaoonekana kuwaunga mkono waasi wa SPLM-kaskazini.

Kwa mujibu wa taarifa za AFP msemaji wa jeshi la Sudan Sawarmi Khaled Saad amesema zaidi ya waasi 700 waliushambulia mji waTalodi, mashariki mwa mji mkuu wa jimbo la Kadugli.

"Wanajeshi waliwasubiri wavamizi waingie katika maeneo matatu wakiwa katika magari kadhaa, lakini katika kipindi cha saa moja wanajeshi walikabiliana na wavamizi hao na kuwashambulia vikali" alinukuliwa akisema hayo.

Lakini msemaji wa waasi hao wa SPLM-kaskazini ameiambia BBC kuwa ni waasi wawili tu waliouawa.

Kusini mwa Kordofan ni moja ya maeneo matatu yanayopakana na Abyei na Blue Nile kukabiliwa na mzozo tangu Sudan Kusini kuanza kujitawala.

Maelfu ya watu wamekimbia mapigano katika maeneo hayo matatu.

Sudan iliwasilisha malalamiko katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Agosti, ikiishutumu Sudan Kusini kwa kuwaunga mkono waasi.

Chama cha SPLM, kinachotawala Sudan Kusini kinakanusha madai ya Jamhuri ya Sudan, licha ya kuwa kiliwaunga mkono waasi wa kaskazini wakati wa vita vya Sudan vya wenyewe kwa wenywewe vilivyochukuwa miongo mingi.