Waafrika wanaimani na uchumi wao

Utafiti wa shirika la BBC unaonyesha kuwa nchi za Afrika zina matarajio makubwa kuhusu uchumi wao kuendelea kukua kuliko maeneo mengine ya dunia.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption China imewekezea sana Afrika

Kwa wastani asilimia 59 ya Waafrika waliohojiwa wanatabiri kuwa hali ya uchumi kwa miezi 12 ijayo itakuwa nzuri, wakati asilimia 14 tu wanasema wanatarajia wakati mbaya wa kiuchumi barani humo.

Mtazamo huu chanya kuhusu hali ya uchumi umeonekana kuwa hivyo katika nchi zote nne yaani, Nigeria, Kenya, Ghana na Misri zilizofanyiwa utafiti huu.

Nigeria imeibuka kuwa nchi yenye uwiano wa juu kabisa wa matarajio ya walaji miongoni mwa nchi zote zilizofanyiwa utafiti kama sehemu ya mataifa 25 yaliyofanyiwa utafiti na Idhaa ya Nje ya BBC.

Mkurugenzi wa GlobeScan Sam Mountford, amesema watu waliohojiwa walikuwa mchanganyiko kutoka mijini na vijijini.

Watu 25,438 walishiriki katika utafiti huo uliofayika kati ya Julai na Septemba mwaka huu. walioshiriki waliulizwa iwapo wanatarajia wakati mzuru au mbaya wa uchumi kwa mwaka ujao, na pia katika miaka mitano ijayo.

Duniani, walaji katika mataifa mengi yenye uchumi mkubwa wana mashaka kuhusu matarajio ya kiuchumi katika nchi zao, wakati ambapo wale katika mataifa yanayoinukia kiuchumi wakiwa na mtazamo wa matarajio mazuri zaidi kwa uchumi wa nchi zao.

Taswira ya muda mrefu zaidi pia inaonyesha kuendelea kupanda kwa matarajio miongoni mwa Waafrika, hususan nchini Misri na Nigeria.

Wamisri ni watu wenye matarajio makubwa zaidi kati ya nchi zote zilizofanyiwa utafiti kuhusu hali ya biashara katika miaka mitano ijayo.