Ghasia zaendelea Syria

Maandamano yaliyofanywa Hama, Syria, Ijumaa Haki miliki ya picha AFP

Watu wane zaidi wanaarifiwa kuuwawa leo asubuhi nchini Syria, kwa mujibu wa wanaharakati wanaopinga serikali ya Rais Assad, na kwamba jana watu 27 waliuwawa.

Ghasia bado zinaendelea siku nne baada ya serikali ya Syria kutangaza kuwa imekubali mapendekezo ya amani ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, na kwamba itaondoa majeshi yake mitaani.

Mapendekezo ya mpango wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu ni kwamba ghasia zisite haraka Syria, na wanajeshi wa serikali waondoshwe mabarabarani.

Hayo hayakutokea.

Vikundi vya upinzani vinasema tangu mpango huo kukubaliwa na serikali siku ya Jumatano, mapiganao yamezidi katika mji wa Homs, shina la upinzani, na watu 23 waliuwawa Jumamosi.

Serikali inaripoti vifo piya, na imesema askari wake 22 wameuwawa hivi karibuni huko Homs, Dara na nje ya Damascus.

Inaelekea Rais Assad anadharau mapendekezo ya Jumuiya ya nchi za Kiarabu, na badala yake ametoa mapendekezo yake mwenyewe: amesema anawapa miezi miwili wanajeshi walioasi kurejea makazini; na raia wasalimishe silaha walizonazo.

Inavoelekea baada ya siku chache Jumuiya ya nchi za Kiarabu itabidi kutangaza kuwa juhudi zao za kuleta amani Syria zimeshindwa; na huenda ikaitoa kwenye jumuiya.