Raia watoa pesa kumsaidia msanii

Ai Wei Wei Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ai Wei Wei

Maelfu ya raia wamechangisha fedha kumsaidia msanii mashuhuri wa China Ai Wei Wei kugharamia kodi ya dola milioni 2.4 anayodaiwa na serikali ya nchi hiyo.

Raia wengi akiwemo mchoraji huyo mashuhuru wanaamini kwamba amelazimishwa kulipa kodi hiyo kutokana na msimamo wake wa kuikosoa serikali ya Uchina.

Karibu watu elfu 20 wamechangia fedha hizo baadhi wakituma hundi, pesa taslimu na hata wengine wakarusha fedha zao ndani ya makaazi ya msanii huyo mjini Baijing.

Ai Wei Wei amesema kampeini hiyo siyo ishara tu ya kuchangisha fedha za kumusaidia bali ni ishara ya hisia za raia ambao wameghadhabishwa na jinsi anavyotendewa.

Utawa wa China umemlaumu kwa kukwepa kulipa kodi ya kima cha $4m.

Hata hivyo wengi wanaamini deni hilo limechochoewa kisiasa ili kumadhibu kwa kuikosoa serikali.

Ai Wei Wei amesema hajaamua ikiwa atalipa kodi hiyo.

Endapo atatumia fedha hizo za raia huenda akashtakiwa kwa kutumia fedha zilizochangishwa kinyume cha sheria kulipa kodi.

Hata hivyo wafuasi wake wamesema serikali inafanya kila jambo kumdhulumu msanii huyo.