Watu wamchangia msanii Weiwei

Msanii Ai Weiwei Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Msanii Ai Weiwei

Maelfu ya watu wamechangisha pesa kulipa kodi kubwa aliyoagizwa msanii wa Uchina Ai Weiwei aiilipe.

Kufikia Jumatatu kiasi cha dola 790,000 kilikuwa kimechangishwa pesa ambazo zitatumiwa kulipa kodi na faini za kiasi cha dola milioni 2.4 ambazo serikali inasema inamdai.

Watu wamekuwa wakitoa pesa kwa kuziweka moja kwa moja katika akaunti yake wengine wakitumia posta na wengine hata kuzirusha nyumbani kwake.

Msanii huyo alikuwa amenuia kulipa pesa hizo baadae sana.

Mchango ulianza tu mara alipotangaza kuwa ametakiwa alipe kodi ya kiasi hicho na serikali yake.

Kwa mujibu wa mtandao wa Twitter ulionukuliwa watu wasiopungua 20,000 tayari wametoa pesa.

Wafanyakazi wake wamepata pesa zilizotiwa kwenya bahasha zilizokunjwa mfano wa ndege na kurushwa uani kwake anakofanya kazi na kuishi.

"Michango hii sio kuhusu pesa tu, ni kuhusu hisia za watu kuhusu kilichofanyika" alisema msanii huyo ambaye aliwataka watu wamemkopeshe pesa kulipa deni hilo.

"Naweza kusema kuwa nimeridhishwa na kuguswa sana na vitendo vyao." Kodi hiyo inahusisha malipo yaliocheleweshwa na faini kuhusu kampuni moja inayoshughulika na masuala ya usanii.

Ingawa Bw. Ai alikuwa anashughulikia masuala ya mipango na mitindo katika kampuni hiyo, vyombo vya utawala vimeshikilia kuwa yeye ndiye alikyekuwa na jukumu kubwa katika kampuni hiyo.

Bw. Ai alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Beijing alipokuwa anajaribu kuondoka nchini humo na kuzuiliwa kwa miezi mitatu.

Aliachiwa bila mashtaka mwezi Juni lakini akashtakiwa kwa kukwepa kodi.

Akizungumza na BBC wiki jana Bw. Ai alisema madai haya ni kisingizio tu anasema anaonewa kutokana na msimamo wake wa kisiasa.