Msafara kutoka Libya wakamatwa Mali

Ramani ya Mali
Image caption Ramani ya Mali

Waziri wa Ulinzi wa Mali Mahamadou Karidio amesema jeshi la Niger limekabiliana na msafara uliokuwa umesheheni silaha kutoka Libya kuelekea Mali.

Mahamadou Karidio amesema kuwa mwanajeshi mmoja ameuawa katika mapambano siku ya Jumapili na wavamizi kadhaa wamekamatwa.

Bw.Karidio hakufafanua kama msafara huo ulikuwa wa wapiganaji wa Libya wafuasi wa serikali iliyong'olewa mamlakani ama walikuwa wanamgambo walio na uhusiano na mtandao wa al-Qaida katika eneo hilo.

Makundi yote yamekuwa yakisafiri kutumia eneo hilo lililompakani ambalo halionekani kuwa na ulinzi wa kutosha.

Eneo hilo la jangwa pia linakabiliwa na uwaasi wa kundi la kikabila la Tuareg ambao baadhi yao walipigana kumuunga mkono Rais aliyeuawa wa Libya Muammar Gaddafi wakati wa mzozo wa Libya.

Serge Hilpron, mkuu wa radio Nomad, iliyo kaskazini mwa Niger ameliambia shirika la habari la AP kuwa duru zake zimemfahamisha kuwa raia wa Libya na wale wa kabila la Tuareg walikuwa katika msafara huo. "Kutokana na tatizo la Libya, kwa sasa kuna walanguzi wanaoelekea Libya kuchukuwa silaha zilizoachwa nyuma na kuzileta hapa.Watu hawa huuza silaha hizi kwa lile kundi la AQIM," Serge Hilpon amesema.

Bw.Karidio amesema wanajeshi wamewakamata baadhi ya wapiganaji katika eneo la Arlit.

Mwanajeshi mmoja ameuawa na wengine wanne kujeruhiwa katika mapigano hayo, alisema.

Bw. Karidio aliongeza kusema kuwa silaha nyingi zimekamatwa ikiwa nipamoja na magurunti na bunduki.

Wataalamu wa ulinzi wanaamini AQIM -ambao huwashambulia na kuwateka wageni katika eneo hilo zima wanapata silaha kutoka Libya ambayo wanaieleza kuwa soko la silaha.

Taarifa za mwezi jana zilisema mwanae Kanali Gaddafi Saif al-Islam, alikuwa katika msafara uliokuwa unaelekea katika jangwa la Libya linalopakana na Niger lakini taarifa hizo hazikuthibitishwa.