Tunakaribia kupata chanjo ya Malaria

Mbu wanaosababisha Malaria Haki miliki ya picha Wikimedia Commons
Image caption Mbu wanaosababisha Malaria

Njia inayotumiwa na vijidudu vinavyosababisha Malaria kali kuingia kwenye chembechembe nyekundu za damu imegunduliwa na watafiti wa taasisi ya Sanger iliyoko Cambridge.

Wanasayansi wanaohusika wanasema kuwa ugunduzi huu unaleta matumaini ya kutengenezwa chanjo ambayo inaweza kusaidia kukabiliana na Malaria vilivyo.

Wataalamu wengine wamesema ugunduzi huu umewashtua na kuwafurahisha wengi.

Maradhi ya Malaria huwatatiza watu milioni 300 kila mwaka.

Katika bara la Afrika, Kusini mwa jangwa la sahara watu milioni moja hufa, wengi wao watoto.

Kuna vijidudu vingi vya Malaria kimoja kinachojulikana kama Plasmodium falciparum ndio chenye makali zaidi na watafiti katika taasisi hiyo wanasema ilikuwa ni utafiti uliohitaji utaalamu wa hali ya juu kugundua kinaingia vipi katika damu.

Kijidudu hicho kinauwezo wa kuepuka na kushinda chanjo nguvu, ambapo katika muda wa dakika tano baada ya mtu kung'atwa na mmbu aliye na kijidudu hicho, viini vyake husambaa na kujificha katika ini.

Baadae hujitoa kwa awamu kadri ya vinavyokuwa na kushambulia chembechembe nyekundu za damu na kuanza kuzaana.

Utaratibu wa mwili wa binadamu kukabiliana na magonjwa hutatizika kuikabili Malaria na watafiti wamekuwa na wakati mgumu kuhusu hilo katika maabara zao.

Image caption Matibabu ya Malaria

Hadi sasa hakuna chanjo rasmi iliyoidhinishwa kukabiliana na Malaria. Majaribio yaliofanywa kwa watu wengi kuhusu vijidudu vingine ambavyo pia vina makali kiasi, yalisababisha kupungua kwa hadi nusu hatari ya kuambukizwa Malaria.

Utafiti huu uliochapishwa katika jarida la "Nature" uliangalia tu vijidudu vinavyoshambulia chembechembe nyekundu za damu.

Watafiti walikuwa wanatafuta proteini katika vijidudu hivyo vya Plasmodium na pia katika chembechembe nyekundu za damu ambazo hushambuliwa na vijidudu hivyo.

Timu hiyo ya watafiti katika taasisi ya Sanger iligundua kuwa "basigin" ambayo huwa juu ya chembechembe nyekunduza za damu na "PfRh5"- proteini inayopatikana katika vijidudu hivyo ni muhimu.

Vijidudu vyote vilivyofanyiwa majaribio na kuvuruga uhusiano kati ya "Basigin" na "PfRh5" vilionesha kutoa ulinzi thabit kwa chembechembe nyekundu dhidi ya mashambulizi.

Mmoja wa watafiti Dkt Julian Rayner, amesema: "Tumeweza kuzuia uvamizi wowote kwa kutumia mbinu mbalimbali, kwa kutumia chembechembe hai kukabiliana na vijidudu hivi kunaweza kukomesha kushambuliwa kwa chembechembe nyekundu za damu."

Mpango uliopo ni wa kutengeneza chanjo ambayo itaimarisha utaratibu wa kukabiliana na magonjwa mwilini utakaoweza kushambulia vijisdudu vya PfRh5.

Mtafiti mwengine katika ugunduzi huu Dkt Gavin Wright amesema chanjo hii itakuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na vijidudu vinavyolengwa kutokomezwa.

Prof Adrian Hill, Mkurugenzi wa taasisi ya Jenner katika chuo kikuu cha Oxford, amesema kuwa baada ya miaka 25 ya utafiti wa Malaria ameridhishwa sana na ugunduzi huu.

Amesema kuwa katika vitabu na utafiti wa wasomi imeelezwa kuwa njia moja ikifungwa ama kuzibwa vijidudu hutafuta njia nyengine.

Aliongeza:"kwa sasa tusubiri kuona itakuwa rahisi vipi kuipata hiyo chanjo lakini kwa sasa hicho kijidudu kinaongoza katika orodha yetu ya mambo ya kushughulikiwa".