Mkutano wa dharura kujadili Syria

Mawaziri wa jumuia ya nchi za Kiarabu wanafanya mkutano wa dharura leo kujadili ghasia zinazoendelea nchini Syria. Mkutano huo utafanya tathmini ya jibu lao juu ya kushindwa kwa Syria kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati yake na Jumuia ya Kiarabu majuma mwili yaliyopita.

Mkutano huo unafanyika kwenye makao makuu ya Jumuia ya nchi za Kiarabu mjini Cairo.

Jumuia hio inakabiliwa na shinikizzo za kuiondoa Syria kutoka uwanachama wa Jumuia baada ya kushindwa kuchukua hatua yoyote kutekeleza mpango wa amani uliokubaliwa baina ya Jumuia na Syria.

Chini ya makubaliano hayo Syria ilitakiwa kuondoa vifaru vyake vya kijeshi kutoka mitaani na kukomesha ghasia dhidi ya waandamanaji.

Lakini badala ya kutekeleza mpango wa amani inaonekana kuwa malumbano yameongezeka ambapo mamia ya raia wameuawa tangu makubaliano hayo.

Na kuna tatizo juu ya kama kuifukuza Syria kutoka Jumuia kutasaidia katika kuleta mabadiliko yoyote. Serikali ya Syria inadai kuwa inautekeleza mpango huo wa amani, na imejitolea kuualika ujumbe kutoka Jumuia ya nchi za Kiarabu kujionea wenyewe - -na hilo linaweza kuwa hatua ya kwanza katika makubaliano.

Hata hivyo baadhi ya nchi za Kiarabu ambazo zinaunga mkono waandamanaji zimeanza kuchikua msimamo wa kwamba haziwezi kuendelea kupuuza hali inayoendelea nchini Syria, bila kutishia kuwepo kwa utulivu katika nchi zao mbali na Syria.