Vijana wa ANC kuamua mstakabali wao

Wafuasi wa Julius Malema Haki miliki ya picha BBC World Service

Hii leo macho yote yanalenga mkutano ambao umeitishwa na umoja wa vijana tawi la chama tawala Afrika Kusini ANC. Kikao cha leo kinajiri baada ya kamati ya nidhamu kumtema nje kiongozi wa vijana Julius Malema na baadhi ya maafisa wengine wa umoja huo.

Malema na wenzake walisukumwa nje kwa kati ya miaka mitano na mitatu kwa kuzua mgawanyiko ndani ya chama cha ANC baada ya kuchochea mageuzi ya utawala nchini Botswana. Wafuasi wa Malema wamekosoa hatua ya kamati hiyo na kiongozi huyo ameapa kukata rufaa.

Julius Malema na wenzake ambao walisukumwa nje wameapa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa kamati ya nidhamu ya ANC.

Hata hivyo huenda maajaliwa ya vijana hawa kufanikiwa katika rufaa yao yakawa hafifu sana kwani wanakamati wengi wanaegemea upande wa rais Jacob Zuma.

Tayari migawanyiko imejitokeza ndani ya tawi hilo la vijana wa ANC. Duru zinasema kwenye kikao maalum cha wiki jana, wafuasi wa Julius Malema walizuiwa dhidi ya kumshambulia mweka hazina waliyemshtumu kuwasaliti.

Kundi jingine katika baraza kuu linadaiwa kuanza kutathmini mustakabali wa tawi hilo bila uongozi wa Julius Malema.Aidha wengine hawaoni haja ya waliofukuzwa chamani kukata rufaa.

Katika uamuzi wake, mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ya ANC Derek Hanekom alisema uamuzi wao ulikuwa wa maadili na siyo shinikizo za kisiasa. Alisema chama hicho hakitakubali ukosefu wa maadili kwani hiyo ilikuwa kama maasi na kinyume cha katiba ya chama.

Miongoni mwa wanasiasa wanaomuunga mkono Malema ni waziri Tokyo Sexwale aliyekosoa uwamuzi wa kamati ya nidhamu. Waziri huyo, ambaye ameonyesha nia ya kuwania urais amesema uwamuzi wa kuwafukuza chamani vijana haistahili. Wadadisi wa siasa Afrika Kusini wamesema hatua hii ni sawa kutangaza kwamba yeye ni hasimu mkubwa wa rais Zuma.

Tawi la vijana la ANC limeeleza waziwazi kumtaka Rais Zuma kuachia ngazi na badala yake naibu Rais Kgalema Motlanthe achukue usukani.

Hata hivyo huenda hilo likasalia ndoto tu ikiwa uamuzi wa kamati ya nidhamu kuwafungia nje Julius Malema na wenzake utasimama, kufikia kongamano kuu la chama cha ANC mwaka ujao ambapo rais Zuma atajitupa ulingoni tena kuteuliwa kuipeperusha bendera ya ANC katika uchaguzi wa urais.