JOSEPH KABILA

Kabila Haki miliki ya picha
Image caption Kabila - anaomba muda zaidi wa kulipa deni kwa wananchi

"Ni kijana na anawakilisha mustakabali wa nchi," Ndivyo walivyosema wafuasi wa Joseph Kabila wakati akiwasilisha fomu ya kugombea urais kwa muhula wa pili mwezi Septemba.

Akiwa na miaka 40, rais huyo anayetetea kiti chake ndio mgombea mwenye umri mdogo zaidi, ingawa tayari amekaa madarakani kwa miaka 10.

Alikuwa kamanda aiye na makuu katika jeshi, wakati baba yake Laurent-Desire Kabila alipouawa mwaka 2001, na aliteuliwa na watu wa karibu na utawala wa baba yake kuongoza DRC wakati huo ikitikiswa na mizozo mbalimbali ya wapiganaji.

Baadaye mwaka 2006 Bw Kabila alipata ushindi katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa kidemokrasia tangu uhuru.

Rais Kabila anaungwa mkono zaidi katika eneo la mashariki ambapo ndio alikozaliwa.

Alipata uungwaji mkono kidogo sana kutoka kwa wapiga kura wa upande wa magharibi katika uchaguzi wa mwaka 2006, huku wanaharakati wengi wa upande wa upinzani wakimtuhumu, bila ushahidi wowote, kuwa ni mzaliwa wa nchi jirani ya Rwanda, nchi ambayo imeivamia mara mbili DRC.

Bw Kabila alikulia nchini Tanzania na anazungumza Kiswahili na Kiingereza vizuri zaidi kuliko lugha zinazozungumzwa zaidi mjini KInshasa, yaani Kilingala na Kifaransa, lugha ambazo alilazimika kujifunza akiwa madarakani.

Kwa muda mwingi akiwa madarakani amekuwa kimya, akivunja ukimya huo tu wakati akizindua kampeni yake ya uchaguzi kwa kufanya mkutano na waandishi wa habari kwa muda wa saa tatu.

"Hatutapoteza uchaguzi huu. Nina uhakika na watu wetu, wameshuhudia jitihada na kujitolea," alisema.

Kampeni ya Bw Kabila ina msemo usemao "Maeneo matano ya ujenzi katika jamhuri", akiwa na maana ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ya nchi, hasa ujenzi wa barabara na vituo vya nishati.

Lakini wananchi wengi wa Kongo wanalalamika kuwa kasi ya maendeleo ya kijamii ni ndogo mno.

Rais Kabila amekiri kuwepo kwa jambo hilo, akisema ana deni la kulipa kwa wapiga kura wa DRC na anawataka wamchague tena ili apate nafasi ya kulipa deni hilo.