Papa awasihi viongozi wa Afrika

Papa Benedict ambaye anazuru Benin, Afrika Magharibi, ametoa wito kwa viongozi wa Afrika, wasiwanyime watu wao matumaini.

Haki miliki ya picha AFP

Papa aliwasihi viongozi wa kisiasa kuweka mfano, na siyo kuwazinga watu wao kufikia malengo yao.

Alisema hayo katika ikulu mjini Cotonou.

Alisema kuna ghasia na rushwa nyingi duniani:

"Wakati huu, kuna kashfa nyingi na uonevu, rushwa nyingi na uroho.

Makosa mengi na uongo, ghasia nyingi ambazo zinaleta mateso na vifo.

Maafa hayo bila ya shaka yako katika bara lenu, na piya yako katika sehemu nyengine za dunia.

Watu wote wanataka kuelewa maamuzi ya kisiasa na kiuchumi ambayo yanafanywa kwa niaba yao.

Wanaona kuna ujanja, na wakati mwengine wanalipiza kwa kishindo."

Papa piya atatoa hotuba ya mapendekezo yake kuhusu mustakbali wa kanisa barani Afrika, baadae katika mji wa Ouidah, shina la imani ya jadi ya "vodoo" nchini humo.

Piya anatarajiwa kuzungumza juu ya uhusaino baina ya ukatoliki na imani za jadi.