Papa Benedict aaga Afrika

Papa Benedict amemaliza ziara yake Afrika, kwa kuongoza sala katika uwanja mkubwa wa mpira mjini Cotonou, nchini Benin, Afrika magharibi.

Maelfu ya waumini katika uwanja wa mpira walimkaribisha papa kwa hamu.

Wanawake na wanaume kwenye mavazi mazuri ya rangi, waliimba nyimbo za dini, huku wakiyumba kwa midundo ya Kiafrika.

Maaskofu zaidi ya 200 wa Afrika piya walihudhuria, pamoja na makasisi mamia kadha wa Benin.

Ingawa joto lilikuwa jingi, hata hivo Papa Benedict, mwenye umri wa miaka 84, ameimudu safari yake ya siku tatu, ambapo alitoa mwongozo mpya kwa kanisa Katoliki Afrika.

Tofauti na Ulaya, kanisa hilo linazidi kukuwa Afrika, ingawa piya linakabiliwa na changamoto kutoka madhehebu ya kiavanjalisti.

Wakati wa sala hiyo Papa alitoa salamu maalumu kwa Wafrika wanaougua UKIMWI na magonjwa mengine.

Lakini alihepa kutaja moja kwa moja matumizi ya condom kama njia ya kupunguza maambukizo ya HIV Afrika.

Malalamiko yake kuhusu condom katika safari yake Afrika miaka miwili iliyopita, yalisababisha utatanishi.