Watu wasiopungua 33 wafa katika ghasia Misri

Waandamanaji Misri Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Waandamanaji Misri

Ghasia zimezuka tena katika Mji Mkuu wa Misri wakati vikosi vya usalama vinajaribu kuwaondoa waandamanaji kutoka medani ya Tahrir mjini Cairo.

Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi wakati waandamanaji waliokuwa katika medani hiyo wakivurumisha mawe na mabomu ya kujiundia ya moto.

Wizara ya Afya inasema kuwa watu 20 walikufa siku ya jumapili na kuongeza idadi ya wote waliokufa kutokana na ghasia hizo kufikia 22 na wengine 1,750 kujeruhiwa tangu ghasia kuanza Jumamosi.

Hatahivyo maafisa wa chumba cha kuhifadhia maiti baadae leo wamesema kuwa idadi ya waliokufa hadi sasa ni watu wasiopungua 33.

Waziri wa utamaduni Emad Abu Ghazi amejiuzulu kutokana na ghasia hizo.

Mena-shirika rasmi la habari nchini humo limesema kuwa Waziri huyo amejiuzulu akipinga njia iliyotumiwa na serikali katika kukabiliana na waandamanaji.

Maandamanao haya ndiyo yamechukuwa muda mrefu zaidi tangu yale ya kumpinga Rais Hosni Mubarak mwezi February.

Waandamanaji wanahofu kuwa jeshi huenda linataka kung'ang'ania madaraka.

Baraza hilo, linaloongozwa na Field Marshal Mohamed Tantawi, linajukumu la kusimamia nchi hiyo wakati inaingia katika demokrasia baada ya miongo mitatu ya utawala wa kimabavu chini ya Bw. Mubarak.

Waandamanaji walisikika wakimtaka ajiuzulu katika maandamano hayo ya mwishoni mwa wiki.

"Wanajeshi waliahidi wataachia madaraka katika kipindi cha miezi sita" mmoja wa waandamanaji hao alisema."sasa miezi kumi tayari imeshapita na bado hawajatimiza ahadi zao, tunaona kama wanatuhadaa"

Umati wa watu ulionekana kuingia katika uwanja wa Taharir hii leo wakipuuza majaribio ya vikosi vya usalama ya kutaka kukomesha maandamano katika uwanja huo uliotumika wakati wa maandamano dhidi ya Hosni Mubarak mapema mwaka huu.

Picha za televisheni zimeonesha gesi ya kutoa machozi ilifyatuliwa kuwalenga waandamanaji ambapo nao waandamanaji walitumia mabomu ya kujiundia ya moto na kuwavurumishia mawe polisi.

Katika ghasia za usiku hospitali ya kujiundia ya mabanda, moja kati ya nyingi zilizowekwa katika medani ya Tahrir ilishambuliwa na polisi.

Na wakati ghasia zikiendelea leo asubuhi, gesi ya kutoa machozi iliyofyatuliwa na polisi inasemakana iliteketeza jumba moja lilikokuwa karibu.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ghasia Misri

Walioshuhudia wanasema watu walishikwa na taharuki wakati mamia ya wanajeshi na polisi walipoanza kuwapiga waandamanaji wakati wakiwafurusha kutoka medani ya Tahrir. Waliojeruhiwa walipelekwa katika zahanati za kujiundia zilizokuwa barabarani na katika misikiti inayouzunguka uwanja huo.

Baadhi ya waandamanaji walionesha risasi za moto zilizotumiwa na kuvishutumu vikosi vya usalama kwa kutumia risasi za moto dhidi yao , dai ambalo linakanushwa na Polisi.

Ghasia kama hizi pia zimefanyika katika miji mingine mwishoni mwa wiki ikiwa nipamoja na Alexandria, Suez na Aswan.

Mwandishi wa BBC Yolande Knell akiwa mjini Cairo anasema matakwa ya waandamanaji yamekuwa yakibadilika badilika. Watu walikuwa wamekusanyika siku ya Ijumaa kulitaka jeshi kuweka tarehe ya kuachia madaraka. Sasa Knell anasema wanawataka viongozi wa kijeshi wajiuzulu mara moja na kuachia madaraka kwa utawala wa kiraia.

Taarifa kutoka baraza la mawaziri siku ya Jumapili ilisema uchaguzi ambao unatarajiwa kuanza katika kipindi cha wiki moja utaendelea na vile vile taarifa hiyo ilipongeza ustahamilivu wa vikosi vya wizara ya mashauri ya ndani wakati wa kukabiliana na waandamanaji.