Vikwazo vipya kwa Iran

Marekani, Uingereza na Canada wametangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran huku kukiwa na wasiwasi juu ya mpango wake wa nuklia.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wazir Hillary Clinton atangaza vikwazo dhidi ya Iran

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani amezungumzia kuhusu "hatua muhimu ya kuongeza shinikizo" kwa Iran.

Awali Uingereza ilisema inakatiza uhusiano na mabenki yote ya Iran, huku Canada ikisema kuwa inapiga marufuku kusafirisha nje bidhaa zinazotokana na petroli,mafuta na viwanda vya gesi.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeonyesha ushahidi kuwa Iran ina mpango wa kutengeza sila za nuklia, lakini Iran imekanusha hilo.

Serikali ya Iran inasisitiza kuwa mradi wake wa nuklia ni wa matumizi kwa raia pekee.

Ripoti hiyo, iliyotayarishwa na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya nuklia (IAEA), inasema Iran imefanya majaribio "yanayohusiana na kuundwa kwa chombo cha nuklia".

Lakini licha ya ripoti hiyo, suala la Iran halijafikishwa mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuwa Urusi na Uchina wamepinga hatua hiyo.