Upigaji kura waongezwa muda DRC

Haki miliki ya picha
Image caption Ghasia DRC

Muda wa upigaji kura umeongezwa na kuingia siku ya pili katika baadhi ya maeneo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo sehemu ambazo upigaji huo haukufanyika siku ya Jumatatu.

Maafisa wa uchaguzi walisema kuongeza muda huo kunaathiri takriban watu 400 katika nchi hiyo kubwa yenye vituo vya kupigia kura 63,000.

Mbali na hatua hiyo kuchukua muda mrefu, upigaji kura huo uligubikwa na vurugu huku vituo vya kupigia kura vikishambuliwa na watu wenye silaha na wapiga kura wenye hasira.

Ni uchaguzi wa pili tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka minane iliyopita, ambapo watu milioni nne walifariki dunia.

Wote wawili rais Joseph Kabila, mwenye umri wa miaka, 40, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 10, na kiongozi wa upinzani mkongwe Etienne Tshisekedi, mwenye miaka, 78, wamesema wanaamini watashinda.

Bw Tshisekedi amemshutumu Bw Kabila kwa kupanga kuutia hila uchaguzi.

'Kuwepo na utulivu'

Kura zimehesabiwa katika baadhi ya vituo, lakini matokeo rasmi yanatarajiwa kutolewa siku chache baadae.

Mwandishi wa BBC Thomas Hubert aliyopo mji mkuu, Kinshasa, amesema maafisa wa uchaguzi ndio kwanza wameanza kupanga usafiri wa matokeo hayo kupelekwa kwenye vituo vya miji, ambapo matokeo ya awali yanaweza kutangazwa.

Baada ya miongo ya migogoro na ubadhirifu, DRC, nchi ambayo ni theluthi mbili ya ukubwa wa Ulaya ya Magharibi, haina miundombinu kama vile barabara na reli.

Kulikuwa na taarifa za ucheleweshaji kwenye vituo vya kupigia kura siku ya Jumatatu, huku baadhi ya wapiga kura wakiiambia BBC walishindwa kupiga kura kwasababu hawakuona majina yao kwenye daftari la kupigia kura au mtu mwengine alishapiga kura kwa majina yao.

Mwandishi wetu amesema watu wengi ambao hawakuweza kupiga kura wamekasirika.

Takriban watu wanne waliuawa baada ya watu wenye silaha- wanaodhaniwa kuwa kundi waliojitenga- wameshambulia vituo viwili vya kupigia kura katika mji wa Lubumbashi kusini mwa nchi hiyo, ambayo ni ngome ya Bw Kabila.

Kwenye ngome ya upinzani ya Kasai magharibi, vituo 15 vya kupigia kura vinaripotiwa kuchomwa moto na wapiga kura wenye hasira baada ya kukaa kwa muda mrefu.