Mashtaka ya Gbagbo yadhihiri

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Bw Gbagbo

Aliyekuwa rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo anakabiliwa na mashtaka manne ya uhalifu dhidi ya binadamu, mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC imesema.

Anashutumiwa kwa kuwa "aliunga mkono uhalifu japo si moja kwa moja" wa mauaji, ubakaji, utesaji na vitendo vengine vibaya dhidi ya binadamu.

Bw Gbagbo, mwenye umri wa miaka, 66, alitiwa kizuizini huko The Hague mapema siku ya Jumatano baada ya kutolewa Ivory Coast.

Ni wa kwanza aliyekuwa rais kutiwa hatiani kukabiliana na kesi huko the Hague na ICC tangu ilipoanzishwa mwaka 2002.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yamefurahishwa na kukamatwa kwake, lakini pia wameonya kuhusu "haki ya mshindi".

Kuna hofu kuwa hisia hizo zinaweza kuibua wasiwasi zaidi Ivory Coast, amesema mwandishi wa BBC aliyopo The Hague Anna Holligan.

'Iliyosambaa na iliyopangwa'

ICC imekuwa ikifanya uchunguzi wa ghasia za miezi minne Ivory Coast, iliyoanza baada ya Bw Gbagbo kukataa kumwachia madaraka Alassane Ouattara katika uchaguzi wa rais Desemba 2010.

Waendesha mashtaka wamesema takriban watu 3,000 wamefariki dunia kwenye vurugu za pande zote mbili na kulikuwa na mateso mengine ikiwemo udhalilishaji wa kijinsia.

Bw Gbagbo anatarajiwa kutokea mahakamani kwa mara ya kwanza katika siku za hivi karibuni.

Kabla ya kupelekwa the Hague, alikuwa kwenye kifungo cha nyumbani huko Korhogo kaskazini mwa Ivory Coast tangu mwezi Aprili, alipoondolewa kwa msaada wa majeshi ya Ufaransa na umoja wa mataifa waliofanya mashambulio ya anga.