ICC Libya kujadili kesi ya Saif Islam

Saif al-Islam Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Saif al-Islam

Kiongozi wa mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita na naibu wake wamewasili nchini Libya kufuatia kukamatwa kwa mwanae Kanali Gaddafi, Saif al-Islamu.

Saif al-Islam anatakiwa kwa madai wa uhalifu wa kivita na mahakama hiyo ya ICC.

Timu hiyo ya ICC itajadili ikiwa kama ashtakiwe Hague ama Libya kama inavyotaka hiyo serikali ya mpito.

Ziara hii inatokea wakati baraza jipya linatarajiwa kutangazwa, miezi mitatu baada ya Kanali Gaddafi kung'olewa mamlakani.

Hii itakuwa hatua ya kwanza ya uundaji wa serikali itakayochaguliwa--utawala huu wa muda una jukumu kubwa la kuandaa rasimu ya katiba na kufanya uchaguzi kwa misingi ya demokrasia.

Waziri Mkuu mteule Abdurrahim al-Keib amesema kuwa maeneo yote ya Libya yatawakilishwa.

Bw. Keib alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu na baraza la kitaifa la Libya mwezi jana.

Baraza hilo ni mseto wa makundi mbalimbali yalioungana kumng'oa mamlakani Kanali Gaddafi ambaye aliuawa Sirte alikozaliwa tarehe 20 mwezi October.

Kiongozi huyo wa mashtaka Luis Moreno-Ocampo na naibu wake Fatou Bensouda, wanaongoza ujumbe ambao utakutana na utawala mpya wa Libya.

Hii ni sehemu ya juhudi za pamoja kufuatia kukamatwa kwa Saif al-Islam siku ya Jumamosi alipokuwa anajaribu kukimbilia nchi jirani ya Niger.

Mahakama hiyo ya ICC pia ilitoa agizo la kumkamata mkuu wa ujajusi wa kanali Gaddafi, Abdullah al-Sanussi, ambaye alichukuliwa kuwa mtu wa karibu sana wa Gaddafi na mmoja wa watu waliokuwa wanaogopewa sana.

Serikali ya Libya inasema kuwa Bw. Sanussi, ambaye ameoa nyumba moja na kanali Gaddafi, alikamatwa nyumbani kwa dada yake katika mji wa kusini wa Sabha siku ya jumapili.

"Suala la ni wapi kesi hizo zitafanywa linapaswa kutatuliwa kupitia mazungumzo na mahakama hiyo. Mwishoe majaji wa ICC wataamua, kuna viwango vya kisheria ambavyo vinapaswa kuzingatiwa" alisema Bw. Ocampo.

Saif al-Islam alikuwa mafichoni tangu vikosi vya NTC kuukamata mji wa Tripoli mwezi August.

Bw. Keib ameahidi kuwa Saif al-Islam atatendewa haki katika kesi inayomkabili baada ya wasiwasi kuwa atateswa kutokana na yale mateso aliyoyapata Kanali Gaddafi baada ya kukamatwa Sirte.