Serikali mpya ya Libya yatangazwa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Abdurrahim al-Keib atangaza baraza lake

Kaimu Waziri Mkuu wa Libya ametangaza baraza jipya la mawaziri la mpito, ikiwa ni hatua ya kwanza ya mchakto wa kuundwa kwa serikali itakayochaguliwa na serikali.

Serikali iyo mpya itakuwa na jukumu la kuandika katiba na kufanya uchaguzi wa kidemokrasia kufikia mwezi Juni mwaka ujao.

Waandishi wanasema viongozi walilenga kuzima tofauti ya makundi mbali mbali nchini humo.

Wakati huo huo, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imekubali kuwa mwanae Kanali Gaddafi aliyekamatwa Saif al-Islam ashtakiwe nchini Libya, wala siyo mjini The Hague.

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Luis Moreno-Ocampo amesema kuwa mahakama hiyo ilitoa hati ya kukamatwa kwa Saif al-Islam kwa madai ya kuhusika na uhalifu wa kivita kwa sababu mfumo wa sheria wa Libya usingeweza kushughulikia kesi hiyo.

Alisema kwa sasa hilo si lazima tena, lakini ICC itasaidia katika kesi yoyote.

Makamanda waasi

Kaimu Waziri Mkuu wa Libya, , alichaguliwa na Baraza la Mpito la Kitaifa (NTC) mwezi uliopita.

Baraza la Mpito ni muungano wa makundi pinzani yaliyoungana kwa nia ya kumuondoa Kanali Gaddafi, aliyeuawa kijijini kwake alikozaliwa, Sirte, tarehe 20 mwezi Oktoba.

Bwana Keib alimchagua Osama al-Juwali kama waziri wake wa ulinzi, al-Juwali ndiye kamanda wa mji wa magharibi wa Zintan.

Siku ya Jumamosi, wapiganaji wake walimkamata mwanae Muammar Gaddafi Saif al-Islam.