UN yalaani vifo vya watu Tahrir Cairo

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mmoja wa waandamanaji aliyejeruhiwa katika medani ya Tahrir mwezi Novemba 2011mjini Cairo

Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu Navi Pillay amelaani ‘matumizi ya nguvu kupita kiasi waziwazi’ dhidi ya waandaamanaji nchini Misri.

Bi Pillay ametoa wito wa kufanyika uchunguzi huru kwa vifo vya watu zaidi ya 30 tangu siku ya Jumamosi.

Shutuma dhidi ya Baraza la kijeshi la Misri bado zinaendelea katika medani ya Tahrir licha ya ahadi ya baraza hilo kuharakisha kukabidhi utawala kwa raia.

Vita mitaani bado inaendelea kwa siku ya tano katika mji mkuu Cairo.

"Natoa wito kwa mamlaka nchini Misri kumaliza matumizi ya waziwazi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji katika medani ya Tahrir na maeneo mengine nchini, ikiwemo matumizi ya mabaya ya mabomu ya kutoa machozi, risasi za mpira na za moto," ilisema taarifa ya Bi Pillay, Kamishana Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa.

"Baadhi ya picha zinazotoka Tahrir, zinaonyesha upigaji wa kikatili kwa waandamanaji ambao tayari wameshakamatwa, inatisha sana," aliongeza.

"Ni muhimu kukawa na uchunguzi wa haraka, usio na upendeleo na ulio huru, na kuwajibishwa kwa wale watakokutwa wanahusika na utesaji huo," alisema Bi Pillay.

Vita vya mitaani Jumatano hii mjini Cairo vinalenga jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani karibu na Medani ya Tahrir.

Vikosi vya usalama vimekuwa vikitumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira dhidi ya waandamanaji.

Kumekuwa na ghasia pia katika miji kadhaa ya Misri ikiwemo Alexandria, Suez, Port Said na Aswan.

Ghasia zimeendelea licha ya Field Marshal Mohamed Hussein Tantawi , kiongozi wa Baraza kuu la Kijeshi (Scaf) kutangaza ahadi ya kuharakishwa kwa kuhamisha utawala wa kijeshi kwenda kwa raia.

Alisema uchaguzi wa Rais utafanyika Julai 2012 – Baraza hilo awali lilisema usingeweza kufanyika mpaka huenda mwaka 2012 mwishoni au 2013.

Hatua hiyo, ikiambatana na rasimu ya katiba iliyotengenezwa awali iliyoliweka jeshi na bajeti yake pembeni bila kuguswa na raia, viliwafanya watu waanzishe maandamano katika medani ya Tahrir siku ya Ijumaa.

Katika hotuba yake, Field Marshal Tantawi pia amithibitisha kuwa uchaguzi wa wabunge uliopangwa kufanyika Novemba 28 utafanyika kama ilivyopangwa.

Ghasia hizi ni mbaya kutokea tangu wimbi la maadamano mitaani yaliyomtoa Rais Hosni Mubarak mwezi February, baada ya miongo mitatu.

Mwandishi wa BBC Jon Leyne mjini Cairo anasema awali jeshi lilipochukua madaraka lilipata imani ya wengi wa wananchi wa Misri lakini sasa waandamanaji wanataka jeshi liachi madaraka mara moja.

Baada ya Field Marshal Tantawi kuzungumza, waandamananaji walioko Tahrir waliimba: "Hatuondoki, Ondoka wewe (Tantawi)."

Muandamanaji mmoja ameliambia shirika la habari la AFP: "Tantawi ni Mubarak, nakala yake. Ni Mubarak kwenye sare ya jeshi."