Muasi wai Sudan kusini 'auawa'

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption George Athor

Serikali mpya ya nchi iliyopata uhuru hivi karibuni, Sudan kusini imesema kiongozi maarufu wa waasi George Athor ameuawa.

Makamu wa rais Riek Machar alisema Bw Athor aliuliwa wakati wa mapigano na askari waliokuwa wakipiga doria mpakani baada ya kuvuka akirejea Sudan kusini.

Taarifa hizo hazijaweza kuthibitishwa na chanzo huru.

Athor aliyekuwa jenerali alianzisha uasi Aprili 2010. Mamia wamefariki dunia katika kipindi cha mwaka uliopita wakati watu wake walipopambana na jeshi la Sudan kusini.

Waandishi walisema uasi huo umekuwa tishio kubwa kwa usalama wa nchi, iliyopata uhuru mwezi Julai.

Bw Athor alianza mapambano kabla ya kupigwa kwa kura ya maoni ya kuamua iwapo taifa hilo liwe huru au la , baada ya kushindwa nafasi ya ugavana katika jimbo la Jonglei.

Upande wa kusini ulimshutumu kwa kutumiwa na kaskazini kuchochea ghasia na kurejesha nyuma upigaji kura- mashtaka ambayo maafisa wa kaskazini waliyakana kwa wakati huo.

Alitia saini mkataba wa kusitisha mapigano na serikali huko Juba mwezi Januari, lakini mapigano yakaanza upya baada ya wiki kadhaa.

Mwandishi wa BBC James Copnall aliyopo Khartoum alisema eneo ambalo linasemekena kuwa aliuawa, kata ya Morobo jimboni Equatoria, ni mbali sana na eneo anapofanyia shughuli zake.

Ofisi ya makamu wa rais imedai kiongozi huo wa waasi alikuwa Rwanda, na alirudi Sudan kusini kwa njia ya barabara kuajiri askari zaidi.

Bw Machar alitoa wito kwa wafuasi wa Bw Athor kuweka silaha chini na kujiunga na "harakati za amani na maendeleo".

Msemaji wa kundi la waasi la Bw Athor aliiambia BBC kwamba alizungumza na kiongozi wake siku ya Jumatatu, lakini hakufanikiwa kumpata tangu wakati huo.

Alisema inawezekana Bw Athor alikuwa Rwanda kwa matibabu, lakini alikuwa hana taarifa kwamba aliuliwa, au alikuwa akifanya nini kwenye eneo hilo ambalo limetangazwa kuwa aliuliwa.