Nandos yafuta tangazo la Bw Mugabe

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais Robert Mugabe

Mtungo ya migahawa ya Afrika Kusini imeondoa tangazo la televisheni linalomdhihaki rais wa Zimbabwe Robert Mugabe kama"dikteta wa mwisho aliyebaki".

Nandos ya Afrika Kusini imesema imechukua uamuzi huo baada ya wafanyakazi wake kupata vitisho huko Zimbabwe kutoka kundi la vijana linalomtii Bw Mugabe.

Video hiyo inamwonyesha mtu aliyefanana na Mugabe akiwa na huzuni akila chakula cha jioni mwenyewe katika meza iliyoandaliwa kwa Kanali Muammar Gaddafi wa Libya, Idi Amin wa Uganda na viongozi wengine madikteta walioshafariki dunia.

Mtandao huo unajulikana kwa matangazo yake ya kichepe.

Karaoke na Mao

Nandos ya Afrika Kusini ilisema kwenye taarifa yake, "Tumekuwa na wasiwasi kutokana na jambo hili lililovyochukuliwa kisiasa nje ya Zimbabwe, vikiwemo vitisho dhidi ya utawala, wafanyakazi na wateja wa Nandos ya Zimbabwe."

"Tuna kila sababu ya kuhisi hatua hii ni ya busara kuchukua katika hali hii ya kubadilika na tunaamini hakuna tangazo lolote la televisheni lenye umuhimu mno wa kuhatarisha usalama wa wafanyakazi na wateja wa Nandos."

Video hiyo ambayo inaarifiwa kugharimu dola 370,000 kutengeneza- ilikuwa ni sehemu ya kampeni za kuelekea sherehe za Christmas kwenye televisheni ya Afrika Kusini.

Ilionyeshwa pia bara lote la Afrika-ikiwemo Zimbabwe- kupitia satelaiti, na hivi karibuni duniani kote, na kupata waangaliaji chungu nzima kupitia YouTube.

Katika tangazo hilo la biashara, muigizaji anayecheza nafasi ya Mugabe anaonekana akikumbuka akiwa na furaha na viongozi wengine wa kidikteta huku kukichezwa wimbo wa Mary Hopkins Those Were The Days.

Bw Mugabe anaonyeshwa akipigana kwa bastola ya maji na Kanali Gaddafi, wakitengeneza malaika kwa kutumia mchanga na Saddam Hussein, wakiendesha kifaru cha jeshi na Idi Amin.

Tangazo 'lisilojali hisia'

Nandos ya Afrika Kusini iliamua kufuta tangazo hilo la biashara baada ya wanaomtii Mugabe kutoka kundi la Chipangano kutoa wito wa kuwepo mgomo na hatua nyingine ambazo hazijasemwa dhidi ya kampuni hiyo.

"Tunalaani matangazo kama hayo kwasababu inashusha hadhi ya rais wetu na kuonekana kama mtu asiye na thamani," Kiongozi wa Chipangano Jimmy Kunaka amemwambia mwandishi wa BBC Brian Hungwe mapema wiki hii.

Bw Kunaka alisema Nandos ya Afrika Kusini lazima " iache ujinga wa kumchezea mkuu wa taifa letu na serikali".

"Tuko tayari kumlinda mkuu wa nchi na serikali kwa njia yoyote tunayoweza," aliongeza, bila kufafanua zaidi.

Kulingana na sheria ya Zimbabwe, ni kosa kumtukana rais au kushusha hadhi ya serikali.