Ubalozi wa Iran Uingereza wafungwa

Waandamanaji wakivamia ubalozi wa Uingereza mjini Tehran Haki miliki ya picha Getty
Image caption Waandamanaji wakivamia ubalozi wa Uingereza mjini Tehran

Uingereza imeamuru kufungwa kwa ubalozi wake nchini Iran na kutaka wafanyakazi wa ubalozi huo wawe wameondoka katika muda wa saa 48.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, William Hague, ametangaza hatua ya kufunga ubalozi wake mjini Tehran ikiwa ni siku moja tangu waandamanaji wavamie ofisi za ubalozi wa Uingereza na maeneo mengine ya kibalozi nchini Iran.

Uingereza pia imefunga ubalozi wa Iran mjini London na kuwafukuza maafisa wake wote.

Naye msemaje wa serikali ya Iran ameonya hatua ya Uingereza ya kufunga ubalozi wake nchini humo kuwa ni ya haraka mno, na amesema kuwa Iran itachukua hatua zaidi zinazostahili.

Iran yalaaniwa

Nchi mbalimbali zimelaani mashambulio katika ofisi za Uingereza mjini Tehran.

Miongoni mwao ni Marekani na Ujerumani, huku nyingine zikitishia kufunga balozi zao nchini Iran.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani, Mark Toner, amesema hatua ya Uingereza na mataifa mengine inaashiria kuwa Iran inaendelea kutengwa.

''Hatua ya Tehran inaisababishia nchi hiyo kuendelea kutegwa zaidi na dunia. Ningependa kuongezea kuwa, kwa hakika Uingereza inawaondoa wafanyikazi wa ubalozi wake, Ujerumani na Uchina zimeamrishi mabalozi wake kurudi nyumbani'' Bwana Toner amesema.

Norway ilifunga Ubalozi wake kwa muda mjini Tehran kwa sababu za kiusalama, lakini bado haijawaondoa wafanyikazi wake.