Biden aunga mkono Uturuki kuhusu Syria

Makamo wa rais wa Marekani, Joe Biden, anasema kuwa serikali ya Syria inasababisha mtafaruku katika eneo hilo, ambao unaweza kuchochea fujo kati ya madhehebu.

Haki miliki ya picha AP

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa Marekani, Bwana Biden alisema hayo katika mkutano wa jana na Rais Abdullah Gul wa Uturuki.

Akihojiwa na gazeti la Uturuki, Hurriyet, hapo jana, Bwana Biden alitoa wito kwa Rais wa Syria, Bashar al-Assad, aondoke madarakani, ili utawala ukabidhiwe kwa viongozi wengine kwa amani.

Amesema Marekani iko pamoja na Uturuki katika ule aliosema ni wito unaozidi kupaa, kumsihi Rais Assad wa Syria ajiuzulu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Haki za Kibinaadamu, limeishutumu Syria kwamba imevunja haki sana katika kukandamiza maandamano, na limeutaka Umoja wa Mataifa uchukue hatua zifaazo.