Mapigano makali yazuka Somalia

Haki miliki ya picha online
Image caption Mapigano makali yatokea Mogadishu

Mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, umekumbwa na moja ya mapigano makali kutokea katika miezi kadhaa, kwa kile kinachoonekana kuwa ni kikwazo kikubwa kwa serikali.

Mapigano hayo yalianza baada ya alfajiri kati ya wapiganaji wa al-Shabab na vikosi vya serikali vikisaidiwa na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AU.

Vikosi vya AU vinaarifiwa kutumia vifaru na silaha nzito.

Al-Shabab waliondoka Mogadishu mwezi Agosti na serikali ikatangaza kuwa inaudhibiti mji huo.

Mapigano yametokea katika wilaya za kaskazini za Karan na Huriwa siku ya Alhamis.

Kuna taarifa za majeruhi lakini taarifa za kina hazijapatikana bado.

Inafuatia shambulio la al-Shabab Jumatano kwenye kambi ya kijeshi inayoendeshwa na vikosi vya AU katika mji wa Wadajir kusini mwa Mogadishu.

Eneo hilo kwa kawaida linachukuliwa kuwa salama.

Tangu kundi hilo la Kiislam lilipoamua ‘kujiondoa kama mbinu’ kutoka Mogadishu, kumekuwa na mashambulizi ya kujitoa muhanga katika mji huo.

Shambulio la hivi karibuni lilitokea Jumanne katioka wilaya ya Hodan na kuua takriban watu watano.

Mapema wiki hii al-Shabab walitangaza kubadili jina lao kuwa Imaarah Islamiya.

Mwandishi wa BBC Will Ross, anasema hatua hiyo imeandaliwa kutoa ujumbe kwa jumuiya ya kimataifa kuwa al-Shabab si rahisi kushindwa

Umoja wa Afrika una vikosi 9,000 mjini Mogadishu kuzuia serikali ya mpito inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa isipinduliwe.

Kenya pia imetuma askari wake kusini mwa Somalia tangu mwezi Octoba, kufuatia mfululizo wa utekaji nyara mpakani ikiituhumu al-Shabab kuhusika.

Bunge la Kenya Jumatano lilikubali jeshi la Kenya lijiunge na vikosi vya AU nchini Somalia.

Somalia imekuwa na miongo miwili ya vita na tangu wakati huo hakujawa na serikali thabiti.

Baadhi ya maeneo ya nchi yamekumbwa na ukame mkali mwaka huu.

Haki miliki ya picha online
Image caption Eneo linalodhibitiwa na al-Shabab