Taliban yazungumza na serikali Pakistan

Naibu kamanda wa Taliban nchini Pakistan anasema kuwa mazungumzo yanafanywa baina ya kundi lake na serikali ya Pakistan.

Haki miliki ya picha AFP

Hadi sasa wakuu hawakusema kitu.

Kikundi cha Taliban Pakistan ni tawi la wapiganaji linalolaumiwa kwa mashambulio yaliyouwa watu Pakistan.

Taarifa kuhusu mazungumzo zimekuwako kwa muda.

Sasa taarifa hizo zimethibitishwa na naibu kamanda wa tawi la Taliban nchini Pakistan, Maulvi Faqir Mohammad.

Amesema kuwa mazungumzo hasa yanafanywa katika eneo la kabila la Bajaur, kwenye mpaka na Afghanistan.

Alisema mazungumzo hayo yana muelekeo mzuri, na kwamba wapiganaji wa Taliban 145 wameachiliwa huru ili kuonesha nia njema.

Wapiganaji kwa upande wao, wameahidi kusitisha mapigano.

Naibu kamanda huyo alisema, endapo makubaliano ya amani yatatiwa saini huko Bajaur, basi mikataba itafuata katika maeneo mengine.

Siku za nyuma mazungumzo yaligeuka kuwa nafasi kwa wapiganaji kujizatiti na kujihami zaidi.