Mkutano wa Durban wamalizika

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa uliofanywa Afrika Kusini umemalizika baada ya kufikia makubaliano, ambayo mwenyekiti wake alisema, "yameinusuru kesho, leo".

Haki miliki ya picha AFP

Majadiliano yataanza mwaka mpya yatayopelekea kupata mkataba wa kupunguza gesi utaofuatwa na mataifa yote.

Kikao cha mwisho cha mkutano kilikuwa kirefu mno.

Baada ya malalamiko kuwa mkutano ulizorota, wenyeji, yaani Afrika Kusini, hatimae walijitahidi kupambana na siasa ngumu za mabadiliko ya hali ya hewa.

Matokeo yake ni muafaka ambao umejaribu kumridhia kila mtu.

Mkataba wa Kyoto utaendelea kuwepo na labda Ulaya na wengine watajishirikisha humo, kama zinavotaka nchi zinazoendelea.

Kumepigwa hatua katika madai kwamba misitu ihifadhiwe na kuwa nchi maskini zipatiwe fedha ili ziweze kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

La muhimu zaidi katika muafaka huo, ni kuwa imewekwa njia ya kutafuta mkataba mpya wenye nguvu ya sheria, utaotoa maelekezo ya kupunguza gesi inayozidisha joto ... mkataba ambao utahusu nchi zote duniani.

Mkutano wa Durban peke yake hautodhibiti kuongezeka kwa joto ulimwenguni.

Lakini angalu umeweka njia ya kufuata, iwapo serikali zitaonesha ujasiri.