Ivory Coast yachagua bunge

Ulinzi umezidishwa Ivory Coast wakati wananchi wanarejea tena kupiga kura leo katika uchaguzi wa kwanza, tangu uchaguzi wa rais wa mwaka jana ambao ulizusha tena vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Haki miliki ya picha AFP

Uchaguzi wa bunge unaonekana kama mtihani kwa nchi inayojaribu kujitoa kwenye mitibuko ya hivi karibuni.

Chama cha rais wa zamani, Laurent Gbagbo, ambaye mwaka jana aliyakataa matokeo ya uchaguzi na sasa yuko kizuizini katika mahakama ya kimataifa, ICC - chama chake kinasusia uchaguzi wa leo.

Rais wa sasa, Alassane Ouattara amesema uchaguzi huo ni hatua muhimu katika kazi ya kuijenga tena Ivory Coast.

Uchaguzi huu hauna matatizo kwa vyama vya serikali ya mseto - uwanja ni wao, kwa sababu vyama vingi vya upinzani havitaki kupiga kura.

Upinzani umekerwa na kukamatwa kwa viongozi waliokuwa pamoja na Rais Gbagbo, Laurent Gbagbo mwenyewe kupelekwa mahakama ya uhalifu ya dunia, ICC; na kile wanachosema ni hali ya usalama inayotisha.

Wadadisi wataangalia watu wangapi watafuata wito wa upinzani wa kususia uchaguzi.

Uchaguzi wenyewe hauvutii, kwa sababu bunge litalochaguliwa halitakuwa na madaraka makubwa.

Hata hivo, kwa serikali mpya, uchaguzi ukiendeshwa vema na kwa salama, utasaidia kuwaonesha wawekezaji kwamba Ivory Coast imeanza kutengenea na inaweza kuvuka mtihani kama huu wa uchaguzi, miezi saba tu baada ya vita.