ICC yamfutia mashtaka kiongozi wa FDLR

Image caption Kiongozi wa waasi wa FDLR Callixte Mbarushimana afutiwa mashtaka na ICC

Majaji wa uhalifu wa kivita katika mahakama ya The Hague wametupilia mbali mashtaka dhidi ya kiongozi wa waasi raia wa Rwanda aliyekuwa anatuhumiwa kwa mauaji na ubakaji nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Majaji katika mahakama ya ICC wameamuru kuachiliwa kwa Callixte Mbarushimana kwa sababu ya upungufu wa ushahidi wa kuyapa nguvu mashtaka yake.

Waendesha mashtaka wanaweza kukata rufaa lakini lazima wawasilishe ushahidi wa ziada.

Bw Mbarushimana, kiongozi wa waasi wa Kihutu amekana kuamuru wapiganaji wake kuua na kubaka raia mwaka 2009.

Bw Mbarushimana, mwenye umri wa miaka 47, alikabiliwa na mashtaka matano dhidi ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na mengine nane ya uhalifu wa kivita yakiwemo mashtaka ya mauaji, ubakaji, mateso, na matendo ya kikatili na mateso, na uharibifu wa mali.

Alikuwa mwanachama mwandamizi wa kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR) linaloko mashariki mwa DR Kongo

Bw Mbarushimana alikamatwa mjini Paris mwezi Octoba, kufuatilia ombi la ICC.

Baadhi ya viongozi wa FDLR wanatuhumiwa kushiriki katika mauaji ya kimbari ya watu wapatao 800,000 mwaka 1994 ya kabila la Tutsi na wenye msimamo wa kadri nchini Rwanda.

Baada ya kundi lililotawaliwa na watutsi wengi kuchukua madaraka na kumaliza mauaji ya kimbari baadhi ya wanachama wa FDLR walikimbilia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na kuanzisha cheche za miaka ya machafuko katika ukanda huu.

Rwanda mara mbili imetuma viksosi vyake nchini DRC ikisema wanatakiwa kukomesha wapiganaji wa Kihutu wanaotumia utawala wa wa wakongo kushambulia Rwanda.

Hali ilisababisha mgogoro wa miaka sita nchini DRC na vifo vya watu wapatao milioni tano.