Urusi yabadilisha msimamo juu ya Syria

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Serikali ya Vladimir Putin wa Urusi aishutumu Syria

Urusi imesambaza mswada wa azimio kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kumaliza mzozo wa Syria, jambo liloshangaza mataiafa ya Magharibi.

Mswada huo unashtumu serikali ya Syria pamoja na upinzani kwa fujo zilizotokea, lakini hauzungumzii vikwazo.

Mataifa ya Magharibi yanasema pendekezo hilo halionyeshi msimamo mkali dhidi ya Syria lakini wako tayari kulifanyia kazi.

Kwa miezi kadhaa sasa nchi za Magharibi zimetaka baraza hilo kuchukuwa msimamo mkali dhidi ya Syria, lakini Urusi na China zimepinga mapendekezo hayo.

Katika fujo za hivi karibuni nchini Syria, maafisa wa usalama 27 wameripotiwa kuuawa na wale walioasi jeshi la nchi hiyo.

Shirika la kutetea haki za binaadamu lenye makao yake jijini London Syrian Observatory for Human Rights linasema kuwa mauaji hayo yalifanyika katika mkoa wa Kusini wa Deraa.

Kuna vikwazo kwa waandishi wa habari wa kimataifa nchini Syria, na ni vigumu kuthibitisha taarifa hizo.

Umoja wa Mataifa unaamini kuwa zaidi ya watu 5,000 wamefariki dunia katika muda wa miezi saba wa mzozo huo, serikali ya Rais Bashar al-Assad inashtumu magenge yenye silaha kwa mauaji hayo.

Katika mahojiano ya hivi karibuni na shirika la habari la Marekani la ABC, alisema kuwa hajamuamrisha mtu yeyote kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.