Hata Afrika uchumi utayumba - IMF

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mkuu wa IMF Christine Lagarde akihutubia mkutano

Mkuu wa IMF, Christine Lagarde, amesema kuwa kuyumba kwa uchumi katika mataifa yaliyostawi kama vile Marekani na nchi wanachama za Jumuiya ya Ulaya kutaenea kote duniani.

Akizungumza na BBC mjini Lagos,Nigeria Bi Lagarde alisema: "Tayari imeonekana kuwa kukua kwa uchumi katika mataifa yanayostawi kunafifia huku ukuaji wa mtaji ukianguka kabisa."

Alisisitiza kuwa kwa ujumla matokeo haya yasiyoridhisha kwa uchumi yataanza kuonekana wazi hasa kwa mataifa yanayouza bidhaa nje ya nchi.

Bi Christine Lagarde ameeleza kuwa Nigeria kwa mfano ni taifa ambalo linategemea sana uuzaji wa mafuta nje ya nchi. Ikiwa mahitaji ya mafuta kwa ujumla yatapungua lazima bei yake itaanguka na hali hii itavuruga uchumi wa Nigeria moja kwa moja, alisema.

Kiongozi huyo wa IMF alisema kushuka kwa mapato yanayotokana na mafuta kutamaanisha kuwa iwapo kunatokea hali ya ukosefu wa usalama nchini Nigeria, kwa mfano, taifa hilo halitakuwa na pesa za kutosha kununua mahitaji yake ya kujilinda.

Alipongeza Nigeria kwa kukadiria bei yake ya mafuta ghafi kuwa Dola 70 kwa pipa, akisema uamuzi kama huo utahakikisha kuwa taifa hilo halijipi matumaini kupita kiasi.

Hata hivyo alieleza kwamba kwa kulazimika kukadiria bei ya mafuta yake kuwa chini sana hatua za ustawi wa taifa hilo zinapungua.

Juu ya madai ya baadhi ya wakosoaji wa IMF kuwa kwa wakati huu shirika hilo linatilia mkazo zaidi ustawi wa mataifa makubwa kiuchumi na kupuuza yale madogo, Bi Lagarde alieleza kwamba shirika lake halina nafasi ya kupendelea taifa lolote.

Alifafanua kwamba kabla shirika lake kuchukua hatua yoyote linahakikisha kuwa linachunguza uchumi wa taifa husika unavyoendelea, na jinsi uchumi wa taifa hilo unavyojihusisha na uchumi wa mataifa mengine duniani.

Alisema pia kuwa kwa sasa mataifa ambayo yanapaswa kuchukua hatua madhubuti kujikwamua kiuchumi ni Marekani na mataifa karibu yote ya Jumuiya ya Ulaya.

Alipoulizwa kubashiri jinsi uchumi wa Afrika utakavyokuwa miaka kumi kuanzia sasa, Christine Lagarde alisema:

"Takwimu zilizopo na asilimia ya ukuaji wa uchumi zinaonyesha matumaini makubwa kwa Afrika. Wakati ambapo ukuaji wa uchumi kote duniani unaonekana kuwa asilimia nne tunakadiria ukuaji wa uchumi wa Afrika kwa asilimia sita. Hiki ni kiwango cha juu ikilinganishwa na ukuaji wastani wa dunia kwa ujumla.

Kiongozi huyo wa IMF anafanya ziara ya siku tatu Barani Afrika ikiwemo Nigeria na Niger.