Waandishi wa Sweden hatiani Ethiopia

Haki miliki ya picha online
Image caption Johan Persson na Martin Schibbye waandishi raia wa Sweden wamekutwa na hatia ya ugaidi

Mahakama ya Ethiopia imewatia hatiani waandishi wa habari wawili raia wa Sweden kwa kuunga mkono ugaidi.

Vikosi vya Ethiopia viliwakamata Johan Persson na Martin Schibbye miezi sita iliyopita wakati wa mapigano na waasi katika eneo mpakani na Somalia.

Mahakama imeamuru kuwa ‘haiwezekani kuwa’ waliingia Ethiopia kinyume cha sheria kukusanya habari.

Ethiopia inawachukulia waasi wa Ogaden National Liberation Front (ONLF) kama kundi la kigaidi.

Hakimu Shemsu Sirgaga alisema safari ya waandishi hao kutoka London mpaka Ethiopia, huku wakiwa na vituo njiani Kenya na Somalia, shirika la AP liliripoti.

"Wana hatia kwa mashtaka haya, basi, kwa kura ya pamoja," Jaji alinukuliwa akisema na shirika la habari la AFP.

"Wameonyesha kuwa ni waandishi wa habari waadilifu na wenye heshma zao, lakini hatuwezi kuhitimisha kuwa mtu mwenye sifa njema hawezi kujihusisha na vitendo vya kihalifu."

Persson na Schibbye walishtakiwa chini ya sheria ya kupambana na ugaidi nchini Ethiopia na wanaweza kufungwa mpaka miaka 15.

Waandishi wote wawili walionekana kukosa cha kusema wakati wa maamuzi hayo na haikujulikana mara moja kama waliyaelewa maana hakukuwa na mkalimani, AFP linaripoti.

Wakati wa kesi yao, walikiri kuingia Ethiopia kinyume cha sheria na kundi la ONLF lakini wakakana mashtaka ya ugaidi.

Mahakama itatoa hukumu wiki mbili zijazo.

Tangu miaka ya 1970, wapiganaji wa ONLF wamekuwa wakipigania haki za waethiopia wanaozungumza Kisomali ambao wanasema wamekuwa wakitengwa na serikali mjini Addis Ababa.

Upande mmoja wa kundi la ONLF ulisaini makubaliano ya amani na serikali mwaka jana, lakini upande mmoja wa kundi hilo umeendelea kupigana na jeshi.

Makundi ya kutetea haki za binadamu mara kadhaa yameishutumu serikali kwa madhila yanayoendelea kwenye eneo linalokaliwa na waethiopia wanaozungumza Kisomali, mahali ambapo waandishi walihitajika kupewa kibali cha kusafiri.