Vijana wa Sudan Kusini 'Watekwa Nyara'

Image caption Wapiganaji wa Sudan

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na wasi wasi kwamba raia wa Sudan Kusini wanaoishi mjini Khartoum, katika Jamuhuri ya Sudan wanatekwa nyara na makundi ya wapiganaji.

Baadhi ya makundi yenye silaha kutoka Sudan Kusini yamekita kambi mjini Khartoum na kuendeleza maasi dhidi ya serikali ya Sudan Kusini.

Serikali ya Sudan imeshutumiwa kuwa inafadhili makundi hayo ya wapiganaji pamoja na kuamrisha utekaji nyara wa raia wa kusini na kuwasajili wapiganaji zaidi kwa lazima japo imekanusha madai hayo.

Hata hivyo afisa mmoja mkuu katika chama cha Rais wa Sudan Omar al-Bashir aliiambia BBC kwamba madai hayo ''hayana msingi''.

Inahofiwa kuwa madai hayo ya utekaji nyara huenda yakatia dosari zaidi uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Sherehe za uhuru wa Sudan Kusini

Kulingana na viongozi wa Sudan Kusini, vijana wamekuwa wakitekwa na makundi yalio na silaha wakiwa katika vyuo vikuu,mitaani na hata katika nyumba zao.

"Hatua ya uongozi wa Khartoum kuwateka vijana kutoka vyuo vikuu ili wajiunge na jeshi ni ya kusikitisha sana,'' Waziri wa mawasiliano wa Sudan Kusini Barnaba Marial Benjamin alisema. Rabbie Abdelattie, afisa mkuu katika chama tawala cha Sudan cha National Congress alikanusha madai hayo.

Aliambia BBC kuwa serikali ya Sudan inatoa usaidizi mwingi kwa raia wa Sudan Kusini.

Hata hivyo raia wa Sudan Kusini wanaoishi Khartoum wanaamini kwamba maafisa wa serikali wanafahamu kinachoendelea.

Mwanaume mmoja alisema kuwa mjombake alitekwa: '' Yeye si mwanajeshi na hana tajriba yoyote ya kijeshi kwa hiyo nina wasiwasi kwamba hatajua jinsi ya kupigana au hata kujilinda yeye mwenyewe.''

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi, UNHCR, linaamini kwamba kuna karibu raia 700,000 wanaoishi Kaskazini mwa nchi hiyo karibu miezi sita baada ya Kusini kujitenga.

Ingawa shirika hilo halijathibitisha taarifa hizi za utekaji nyara, limeelezea kuwa lina wasiwasi kutokana na ripoti wanazopokea.

Kulingana na msimamizi wa shughuli za usalama wa shirika la UNHCR, Philippa Candler, kumekuwa na watu wanaotembelea nyumba katika baadhi ya maeneo.

''Tumesikia kwamba kuna uwezekano wa watu kuachiliwa iwapo watalipa pesa''.

UNHCR inasema imeelezea serikali ya Sudan wasiwasi wao kuhusu suala hilo.

Shutuma zinalimbikiziwa makundi ya waasi kwa kutekeleza utekaji nyara huo.