Msimamo mkali wa dini wapingwa Israil

Wayahudi wa msimamo mkali wakizozana na wa upande wa wastani Haki miliki ya picha Reuters

Maelfu ya Waisraili wameshiriki kwenye mhadhara kulaani tabia ya Wayahudi wenye msimamo mkali wa dini, ambao wanataka wanawake watengwe mbali na wanaume.

Rais Shimon Peres wa Israil alisema wachache nchini Israil wanafanya vitendo vya aibu na wanavunja umoja wa taifa.

Aliwahimiza watu wajiunge na maandamano hayo katika mji wa Beit Shemesh, karibu na Jerusalem.

Mji huo umezusha hasira nchini Israil, tangu msichana wa miaka minane aliposema anaogopa kwenda shule, baada ya wanaume wa Kiyahudi wenye msimamo mkali kumtemea mate, na kumshutumu kuwa hakuvalia sawasawa.

Mwandishi wa BBC alioko Beit Shemesh anasema mhadhara huo unaonesha jinsi Wayahudi wenye msimamo wa wastani, na wachache wenye msimamo mkali, walivogawanyika juu ya swala ya kulazimishwa kufuata dini kwa namna fulani.