Rais wa Guinea-Bissau afariki dunia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa Guinea-Bissau Malam Bacai Sanha

Rais wa Guinea-Bissau Malam Bacai Sanha amefariki dunia hospitalini mjini Paris, imeripoti redio ya taifa.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 64, aliyepata urais mwaka 2009, alisafiri kwenda Ufaransa kwa ajili ya kupata matibabu mwishoni mwa Novemba baada ya kupelekwa akiwa mahututi.

Maradhi yaliyokuwa yakimkabili hayajaelezwa hadharani lakini ilikuwa ikijulikana kuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.

Bw Sanha awali alikuwa akitibiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwenye hospitali ya nchi jirani ya Senegal.

Amefariki dunia kwenye hospitali ya kijeshi ya Val de Grace kwenye mji mkuu wa Ufaransa.

Rais huyo amekuwa akilazwa mara kwa mara nje ya nchi tangu awe kiongozi wa Guinea-Bissau.

Aliyemtangulia rais, Joao Bernardo Vieira, aliuliwa na askari walioasi.

Nchi hiyo imejikuta kwenye mapinduzi ya mara kwa mara na ghasia tangu kupata uhuru kutoka kwa Wareno mwaka 1974, na imekuwa eneo la kufanya biashara ya dawa za kulevya baina ya Amerika ya kusini na Ulaya.

Mwishoni wa Desemba mkuu wa jeshi la majini, Jose Americo Bubo Na Tchuto, alikamatwa na kutuhumiwa kwa kutaka kuchukua madaraka bila ya kuwepo kwa Bw Sanha.