Amri ya kutotembea yawekwa Nigeria

Amri ya kutotoka nje wakati wowote ule imetangazwa katika jimbo la Adamawa, Nigeria, baada ya mashambulio kadha dhidi ya Wakristo.

Haki miliki ya picha Reuters

Jeshi limeshika zamu mabarabarani, na taarifa kutoka mji mkuu wa jimbo, Yola, zinaeleza kuwa maduka na maofisi yote yamefungwa, na huduma za lazima tu ndio zinaruhusiwa.

Wafuasi wa kikundi cha Waisalmu wenye siasa kali, Boko Haram, wameshambulia kanisa, kituo cha jamii, na duka la msusi katika siku za karibuni, na kuuwa watu kama 29.

Sheria za dharura zilianzishwa katika majimbo kadha mengine ya kaskazini mwa Nigeria juma lilopita, ambako Boko Haram wamefanya mashambulio piya.

Kikundi hicho kimeuwa watu zaidi ya 500 katika muda wa mwaka.