Mechi ya Sao Tome imeahirishwa

Kombe la Mataifa ya Afrika 2013
Image caption Sao Tome kupambana na Lesotho

Mechi ya mkondo wa kwanza kati ya Sao Tome na Lesotho kufuzu kushirikishwa katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2013 imeahirishwa, na sasa itachezwa tarehe 15 mwezi huu wa Januari.

Awali mechi hiyo ilitazamiwa kuchezwa siku ya Jumapili nchini Sao Tome.

Mechi hiyo imeahirishwa baada ya timu ya Lesotho kushindwa kupata ndege kama ilivyotazamiwa, na sasa timu hiyo itasafiri tarehe 12 Januari.

Shirikisho la soka barani Afrika, CAF, limeidhinisha mabadiliko hayo, lakini mechi ya pili itachezwa kama ilivyopangwa, tarehe 22 Januari, mjini Maseru.

Timu ambayo itaibuka mshindi itacheza na Sierra Leone katika raundi ya kwanza ya mechi hizo za kufuzu.

Fainali za Kombe la Afrika mwaka 2013 zitachezwa nchini Afrika Kusini.

Mataifa ya Sao Tome na Lesotho hayakushiriki katika kampeni ya kufuzu kwa mashindano ya mwaka huu wa 2012 ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Sao Tome ilicheza mechi yake baada ya kipindi cha karibu miaka minane dhidi ya Congo Brazaville mwezi Novemba mwaka jana, mechi ambayo ilimalizika kwa sare ya 1-1, mechi ya mkondo wa pili ya kufuzu kwa mashindano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2014.

Hata hivyo, ilishindwa kwa jumla ya magoli 6-1.

Lesotho ilifanikiwa kusonga mbele katika mechi za kufuzu za makundi za Kombe la Dunia mwaka 2014, baada ya kuishinda Burundi kufuatia kanuni ya mabao ya ugenini, baada ya kuwa na jumla ya sare ya magoli 2-2.