Syria yatakiwa iache kutumia nguvu

Ujumbe wa nchi za Kiarabu, waliovaa makoti ya njano, wamezungukwa na waandamanaji  nchini Syria Haki miliki ya picha Reuters

Jumuia ya nchi za Kiarabu imetoa wito kwa serikali ya Syria na makundi yenye silaha yaache haraka kutumia nguvu dhidi ya raia.

Mawaziri wa mashauri ya nchi za nje wakikutana mjini Cairo, wameamua kuwa ujumbe walioutuma Syria kuchunguza hali, uendelee na kazi yake, ingawa wapinzani wamelalamika kuwa hausaidii kumaliza fujo huko.

Mawaziri hao walielezewa ripoti ndefu kutoka kwa kiongozi wa ujumbe wao nchini Syria, na wameoneshwa ramani, michoro na picha kuhusu yale wachunguzi walioshuhudia. Mawaziri hao hawakutaja pendekezo kwamba ujumbe wao uongezwe nguvu kwa kuwajumuisha wataalamu wa Umoja wa Mataifa. Katibu Mkuu wa jumuia hiyo amesisitiza kuwa idadi ya watu waliouwawa imepungua kwa ujumbe wao kuweko nchini Syria.