Uholanzi yapiga marufuku mirungi

Haki miliki ya picha AP
Image caption Matumizi ya Miraa au mirungi yamepigwa marufuku Uholanzi

Serikali ya Uholanzi imetangaza kuwa itapiga marufuku matumizi ya mirungi au miraa.

Ni jani lenye dawa ambalo likitafunwa linatoa juisi ambayo ina visisimuzi vya asili na ni maarufu kwa jamii ya wasomali.

Uholanzi inatumika kama mkondo wa kuingiza na kusafirishia miraa/mirungi kutoka Pembe ya Afrika kwenda nchi za Ulaya.

Kuna wasiwasi kuwa dawa zinaweza kusababisha maradhi ya akili au kuchanganyikiwa.

Mwandishi wa BBC Anna Holligan akiwa Uholanzi anasema nchi hiyo ina utamaduni wa kutoa uhuru kwa dawa baridi

Hata hivyo, ripoti ya serikali ya Uholanzi ilisema kelele, uchafu na tishio kwa umma linalotolewa na watu wanaotafuna mirungi kama baadhi ya sababu za kupiga marufuku dawa hiyo.

'ulegevu na kukosa msaada'

"Nahusika katika kupiga marufuku kwa sababu inaonekana inasababisha matatizo makubwa hasa kwa jamii ya wasomali," Waziri wa Uhamiaji Gerd Leers alinukuliwa akisema katika Radio Uholanzi.

Athari na hatari za Mirungi

  • Watumiaji wanajisikia wako macho, wana furaha na wanaongea sana.
  • Inakata hamu ya chakula.
  • Matumizi makubwa yanaweza kusababisha kukosa usingizi, shinikizo la damu, matatizo ya moyo na kukosa nguvu.
  • Inaweza kusababisha kansa ya mdomo ikiwa itatumika kwa muda mrefu.
  • Inaweza kusababisha kujikia kuwa na wasiwasi, ukorofi na kusababisha hofu na matatizo ya akili.
  • Inaweza kusababisha matatizo ya akili kuwa makubwa zaidi.

Chanzo: www.talktofrank.com

Alisema kuwa 10% ya wanaume kwa Kisomali nchini Uholanzi wawameathirika kwa dawa hizo.

"Wamelegea na wanakataa kushirikiana na serikali au kuwajibika kwa ajili yao na familia zao," Alisema.

Ni raia wachache wa Uholanzi wanaotumia dawa hiyo, ambayo kwa kiasi kikubwa inatafunwa na watu kutoka Somalia, Ethiopia, Kenya na Yemen

Mwandishi wa BBC anasema zaidi ya wasomali 25,000 sasa wanaishi Uholanzi na idadi yao inavyoongezeka na matumizi ya mirungi nchini humo yanaongezeka. Kwa sasa ni halali kuingiza mirungi/miraa kupitia uwanja wa ndege wa Schiphol Amsterdam mara nne kwa wiki. Majani ya mirungi yanatakiwa kuwa mabichi la sivyo inapoteza ladha yake.

Mwaka uliopita, mirungi yenye thamani karibu $18milioni (£11.6m) iliingizwa nchini Uholanzi.

Matumzi ya visisimuzi yamepigwa marufuku Mrakani, Canada na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya.

Lakini bado inapatikana Uingereza ambako inauzwa kihalali katika idadi ndogo ya maduka.