Mkuu wa Boko Haram atetea mashambulio

Shekau Haki miliki ya picha youtube
Image caption Shekau ametetea vitendo vyao

Kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Kiislam wenye itikadi kali nchini Nigeria, Boko Haram, ametetea mashambulio dhidi ya Wakristo ya hivi karibuni, akisema ni ulipizaji kisasi wa kuuawa kwa Waislam.

Katika ujumbe wake wa kwanza kupitia video, ambao umetolewa kwenye wavuti wa YouTube, kiongozi huyo Abubakar Shekau ametaja mashambulio dhidi ya Waislam katika miaka ya hivi karibuni katika maeneo kadhaa kaskazini mwa Nigeria.

Wanamgambo wa Boko Haram walishambulia makanisa kadhaa siku ya Krismasi, na kuua waumini wengi.

Hali ilisababisha kutokea kwa mashambulio ya kulipiza kisasi katika isikiti, hasa katika maeneo ya kusini yenye Wakristo wengi.

Kujitenga

Nigeria, nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika, ikiwa na watu milioni 160, imegawanyika kati ya Waislamu wengi upande wa kaskazini, na kusini ambapo Wakristo na wasio na dini wanaishi.

Maelfu ya watu wamekimbia makazi yao kufuatia mashambulio ya hivi karibuni, na kusababisha baadhi ya watu, akiwemo rais wa Nigeria na kiongozi wa taasisi kuu ya Kikristo, kufananisha na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 1967-70 ambapo viongozi wa kabila la Igbo walipotaka kujitenga.

Bw Shekau, akiwa amevalia kilemba cha rangu nyekundu na nyeupe, pamoja na vazi la kujikinga na risasi na huku amekaa mbele ya bunduki mbili, amesema alikuwa akijibu taarifa za hivi karibuni kutoka kwa rais wa Nigeria Goodluck Jonathan na taasisi kuu ya Kikristo, Christian Association of Nigeria.

Amemuonya Rais Goodluck Jonathan kuwa majeshi ya usalama ya Nigeria hayataweza kuliteketeza kundi hilo.

Bw Jonathan, ambaye ni Mkristo, ametangaza hali ya hatari katika baadhi ya majimbo ya kaskazini, lakini mashambulio yameendelea.

Siku ya Jumanne, watu wenye silaha walishambulia kwa risasi baa moja katika jimbo la kaskazini la Yobe, na kuua watu wanane wakiwemo maafisa wa polisi.

Rais hivi karibuni alisema anawashuku baadhi ya maafisa, wanasiasa na majeshi ya usalama kujihusisha na Boko Haram.

Kidini

Akitetea machafuko ya hivi karibuni, Bw Shekau ametaja mauaji ya Waislamu katika miaka ya karibuni katika maeneo kama Jos, Kaduna, Zangon Kataf na Tafawa Balewa.

Baadhi ya maeneo hayo kumekuwa na kuzuka kwa ghasia za kijamii, lakini waandishi wa habari wanasema mara nyingi huwa ni mizozo ya muda mrefu juu ya rasilimali kama vile ardhi, au wanachochewa na wanasiasa, kuliko kuhitilafiana kwa misingi ya kidini.

Mchungaji Ayo Oritsejafor, rais wa taasisi kuu ya Kikristo ya Nigeria alisema siku ya Jumamosi kuwa wajumbe wake wajizuie dhidi ya mashambulio, ambayo alisema ni "ya mfumo wa kikabila na kuteketeza kidini".

Bw Shekau amesema kundi lake litafanya mazungumzo tu na serikali iwapo itazingatia mafundisho ya Kiislam.

Alisema lengo kuu la kundi hilo linasalia kushambulia majeshi ya usalama, ambayo amesema yalimuua kiongozi wao wa zamani Mohammed Yusuf baada ya kukamatwa mwaka 2009.

Baada ya kukaa kimya kwa muda, mwaka 2010 kundi hilo lilianza mashambulio kwa kutumia magari na pikipiki katika maeneo ya ngome yake katika mji wankaskazini mashariki wa Maiduguri.

Mwaka jana, kundi hilo lilifanya shambulio la kujitoa mhanga katika maeneo makubwa kama vile makao makuu ya Umoja wa Mataifa na polisi katika mji mkuu wa Abuja.