Msimamo wa Kanisa kuhusu kura DRC

Kanisa katoliki lenye wafuasi wengi huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo linatarajiwa kutoa msimamo wake rasmi kuhusu uchaguzi wa mwezi Novemba uliokumbwa na utata.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kiongozi wa UDPS naye anadai ushindi

Msimamo huo unatolewa wakati matokeo rasmi ya uchaguzi wa ubunge yakitarajiwa kutolewa mwisho wa wiki hii.

Hali ya wasiwasi iliofuata baada ya uchaguzi huo ilipungua wakati wa likizo ya krismasi lakini huenda katika siku chache zijazo hiyo hali huenda ikarejea tena.

Kwa muda wa siku tatu maaskofu wa kanisa katoliki wamekuwa wakijadiliana kuhusu kauli hiyo ya pamoja na hatua wanafaa kuchukua baada Rais Joseph Kabila kutangazwa mshindi huku mpizani wake mkuu Etienne Tshisekedi naye pia akijitangaza kama rais wa nchi.

Jumamosi iliopiata katika misa iliotangulia mkutano huo wa maaskofu, kauli iliotolewa ni kuwa wakatoliki nchini humo wanalazimika kuheshimu utawala na sheria zilizo za haki na wala sio ule uliopatikana kwa njia za udanganyifu.

Eugene Banyaku, mhadhiri katika chuo kikuu mjini Kinshasa na mashauri wa Rais Kabila anakiri asilimia 60 hadi 70 ya Wacongomani ni wafausi wa kanisa hilo na kuwa maaskofu hao wanajukumu la kutetea ukweli ila amewaonya dhidi ya kuitisha maandamano.

"suala hilo linafaa kuwa la kubadlishana mawazo na fikra na wala sio mapambano ya mitaani. Ikiwa wataamua kupanga maandamano basi lazima wawe tayari kukabili hali pale wakereketwa wengine ambao sio wakatoliki watakapo teka maandamano hayo" alisema Bw Banyaku

Hayo yakijiri, mikakati ya kujumuisha matokeo ya kura za ubunge inaenedlea kote nchini. Kulingana na Umoja wa Mataifa, theluthi mbili ya matokeo katika jumla ya majimbo 169 yapo tayari.

Matokeo ya awali yanaonyesha chama cha Rais Kabila PPRD, kinaongoza kwa idadi ya wabunge kikifuatiwa na kile cha Bw Tshisekedi cha UDPS.

Ndugu yake Rais Kabila na dadake pamoja na washauri wake wakaribu wamefanikiwa kushinda. Hata hivyo washirika wake wengi hasaa mawaziri walishindwa kwenye uchaguzi huo.

Tume ya uchaguzi imesema matokeo yote ya wabunge yatatangazwa ijumaa wiki hii lakini licha ya hilo matokeo ya miji mikubwa ukiwemo wa Kinshasa bado hayajatangazwa.

.