Mgomo wa Nigeria haukupatiwa dawa

Mazungumzo baina ya serikali ya Nigeria na vyama vya wafanyakazi kuhusu fidia ya bei ya mafuta yamevunjika, na sasa kuna uwezekano mkubwa kuwa wafanyakazi wa visima vya mafuta nao watajiunga na mgomo ulioendelea kwa juma zima.

Haki miliki ya picha AP

Katika mkutano wa jana usiku vyama vya wafanyakazi vilitaka serikali irejeshe kwa ukamilifu fidia ya bei ya mafuta, ama sivyo wataendelea kugoma kesho.

Serikali haikufanya hivo, na inavoelekea mgomo wa watumishi wa serikali, wafanyakazi wa mabenki na wengineo, utaendelea kesho.

Muhimu zaidi ni kuwa wafanyakazi katika visima vya mafuta nao wanatarajiwa kuanza kugoma piya juma lijalo.

Hatua hiyo itazidisha bei ya mafuta katika masoko ya dunia kwa sababu Nigeria ni nchi ya sita duniani zinazotoa mafuta kwa wingi.

Bei ya petroli kwa wananchi wa Nigeria ilikuwa haitimii nusu dola kwa lita moja.

Baada ya serikali kuondosha fidia, bei ikazidi, na lita moja kufikia dola nzima, na kupelekea bei za vyakula nazo piya kupanda.

Serikali ilisema fidia ya bei ya mafuta ikigharimu serikali dola bilioni 8 kila mwaka, ambazo inasema, zinaweza kutumika kujenga miundo mbinu na huduma za jamii.