Mgomo wa Mafuta Nigeria wasitishwa

Image caption Maandamano yasitishwa Nigeria

Vyama vya wafanyakazi nchini Nigeria vimesitisha mgomo wao baada ya Rais kukubali kupunguza bei ya petrol kufuatia wiki nzima ya maandamano.

Mgomo uliitishwa baada ya bei kupanda mara dufu baada ya Rais Goodluck Jonathan kuondoa ruzuku ya mafuta kuanzia tarehe mosi Januari.

Mapema Jumatatu, alitangaza kuwa angerejesha sehemu ya ruzuku hiyo.

Nigeria ni nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa mafuta barani Afrika lakini kwa sehemu kubwa inaagiza mafuta yaliyosafishwa kutoka nje.

Waandishi wanasema raia wengi wa Nigeria wanaona upatikanaji wa mafuta kwa bei nafuu ndio njia pekee ya kunufaika na utajiri huo, ambao umegubikwa na ufisadi wa maafisa.

Vyama hivyo vya wafanyakazi vimesema vimechukua uamuzi huo kuokoa maisha ya watu baada ya kupokea taarifa kuwa vyombo vya usalama vimepewa amri ya kutumia nguvu kumaliza maandamano hayo. Uamuzi huo umekuja wakati polisi na jeshi wakiwa wamesambazwa kwa wingi katika mitaa ya miji mingi.

Polisi katika mji wa kibiashara wa Lagos walifyatua risasi za moto hewani na mabomu ya kutoa machozi kusambaza mamia ya waandamanaji Jumatatu.

Vizuizi vya kijeshi vilionekana katika sehemu za mji kwa mara ya kwanza tangu maandamano yaanze wiki iliyopita.

Mgomo 'umefanikiwa’

Shirikisho la Wafanyakazi wa Nigeria na Muungano wa wafanyakazi nchini humo limewaambia waandishi wa habari mjini Abuja kuwa wamepongeza ahadi ya serikali ya hivi karibuni kupambana na ufisadi katika sekta ya mafuta. Wameelezea siku sita za mgomo kama ‘mafanikio.’

"Tuna uhakika hakuna serikali au taasisi yoyote itawachukulia raia wa Nigeria kwa urahisi tena," alisema Abdulwaheed Omar,Rais wa Shirikisho la wafanyakazi Nigeria.

Rais wa vyama vya wafanyakaiz nchini humo Peter Esele, amekiambia kipindi cha BBC Focus on Africa kuwa vyama hivyo vingekuwa tayari kutafakari juu ya kuondolewa kwa ruzuku hiyo kwa kutumia maandamano, lakini kwanza wanataka kuona serikali inachukua hatua katika matatizo makubwaya miundombinu na nishati.