Kiongozi wa Boko Haram akombolewa

Kiongozi wa Boko Haram Haki miliki ya picha AP
Image caption Kiongozi wa Boko Haram

Idara ya polisi nchini Nigeria, imethibitiha kuwa mshukiwa mmoja ambaye anaaminika kuwa kiongozi wa kundi la Boko Haram, ametoweka, baada ya wapiaganaji wa kundi hilo kushambulia msafara wa polisi ambao ulikuwa ukimpeleka kizuizini.

Mshukiwa huyo alikuwa amekamatwa na polisi siku ya Jumamosi na alikuwa akisafirishwa korokoroni ili kuwapa maafisa wa polisi nafasi ya kufanya uchunguzi zaidi.

Baada ya kukamatwa mshukiwa huyo alikabithiwa kamishna wa polisi, ambaye aliamrisha mshukiwa huyo apelekwe katika kituo kimoja cha siri cha Abaji.

Wakati msafara huo ulipokuwa njiani, wapiganaji wa kundi hilo waliushambulia na kumkomboa kiongozi huyo wa Boko Haram.

Idara ya polisi nchini humo, imesema maafisa wake kadhaa hawakuwajibika na serikali ya nchi hiyo imesimamisha kazi kwa muda kamishna huyo wa polisi.

Ikiwa uchunguzi utabainisha kuwa yeye na maafisa wake walihusika na kutoweka kwa mshukiwa huyo, huenda wakafunguliwa mashtaka ya uhalifu.

Kile ambacho polisi hawajataja ni kwamba mshukiwa huyo, kwa jina Kabir Sokoto, alikamatwa akiwa ameandamana na mwanajeshi katika chumba kimoja cha Gavana wa jimbo la Bornu kilichoko Abuja wikendi iliyopita.

Maafisa wa serikali wa jimbo hilo mjini Maiduguri walithibitisha kukamatwa kwa mshukiwa huyo.

Vyombo vya habari nchini Nigeria vimetangaza kwamba mshukiwa huyo ni afisa wa ngazi ya juu na ndiye anayeaminika kuwa naibu wa kiongozi wa kundi hilo la Boko Haram .