Al-Shabaab washambulia kambi ya Ethiopia

al-Shabaab
Image caption Wapiganaji wa al-Shabaab wanadhibiti maeneo mengi Somalia

Wanamgambo wa Kisomali wamefanya shambulio la kujitoa mhanga kwa kutumia gari dhidi ya kambi ya wanajeshi wa Ethiopia katikati ya Somalia, kwa mujibu wa watu walioshuhudia.

Kundi la al-Shabaab limesema limeua wanajeshi 10 wa Ethiopia katika shambulio hilo katika mji wa Beledweyne, lakini taarifa hizo hazijathibitishwa.

Majeshi ya Ethiopia yaliuteka mji wa Beledweyne kutoka kwa al-Shabaab mwezi uliopita.

Majeshi ya Kenya pia yameingia Somalia kupambana na kundi hilo linalotajwa kushirikiana na al-Qaeda ambalo bado linadhibiti maeneo mengi.

Kiungo muhimu

Beledweyne ni mji uliopo sehemu muhimu, ukiwa kilomita 30 kutoka mpaka na Ethiopia na pia katika barabara kuu inayokwenda mji mkuu wa Mogadishu, huku mji huo ukiwa kiungo muhimu kati ya kusini na kaskazini.

"Kulikuwa na mlipuko mkubwa ambao ulitikisa jiji zima," amsesema Mohammed Osman afisa wa usalama akizungumza na AFP.

"Mlipuaji wa kujitoa mhanga alipigwa risasi na walinzi kabla ya kufika katika lango kuu, na alijilipua ndani ya gari lake. Bado tunafanya uchunguzi," alisema.

Watu walioshuhudia wamesema sehemu kubwa ya jengo ambalo linashikiliwa na majeshi ya Ethiopia limeporomoka.

Mashambulio

Ethiopia imesema inataka kuondoa wanajeshi wake kutoka Somalia na Umoja wa Afrika umesema wanajeshi wake ndio watachukua nafasi yao, ingawa hakuna tarehe kamili iliyopangwa.

Umoja wa Afrika unasaidia majeshi ya serikali mjini Mogadishu. Al-Shabaab iliondoka mjini Mogadishu mwezi Agosti mwaka 2011 lakini imeendelea kufanya mashambulio ya kujitoa mhanga dhidi ya mji huo.

Katika kile waandishi wa habari wa BBC wanasema ni ishara ya kuongezeka kwa imani katika hali ya usalama mjini humo, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa amehamia Mogadishu kutoka Kenya, baada ya miaka 17.

"Nina imani kuwa kuwasili kwa ofisi ya kisiasa ya Umoja wa Mataifa kutaashiria kuanza wa imani mpya ya kustakabali wa Somalia," Balozi Augustine Mahiga alisema katika taarifa yake baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege.

"Tuna mengi ya kufanya na tuna ari ya kuanza kazi mara moja," alisema, akiahidi kuwa kwenda kwao "kutaanzisha enzi mpya ya ushirikiano na majadiliano ya kisiasa wakati kipindi cha mpito kikiwa kinafikia tamati yake".

Kuwepo kwa wanajeshi wa Ethiopia nchini Somalia kulizua utata mwaka 2006-9, hata hivyo, wachambuzi wanasema upinzani umepungua wakati huu na al-Shabaab wamepoteza kuungwa mkono kwa kiasi fulani.

Kundi hilo la wanamgambo limepiga marufuku mashirika ya misaada ya kimataifa katika maeneo inayoyadhibiti ambayo yamekumbwa na ukame.

Maelfu ya watu walikufa katika maeneo yaliyotajwa kuwa yameathirika na ukame.