Serikali Sudan kuwapokonya silaha raia

Wapiganaji wa kikabila walioko katika jimbo la Jonglei Haki miliki ya picha spl arrangement
Image caption Wapiganaji wa kikabila walioko katika jimbo la Jonglei

Serikali ya Sudan Kusini imeahidi kuwapokonya silaha watu wa makabila hasimu kufuatia mapigano makali ambayo yamesababisha vifo vya mamia ya watu katika jimbo la Jonglei.

Waziri wa habari wa Sudan Kusini, Barnabas Marial Benjamin, ameiambia BBC kuwa maafisa zaidi wa polisi wametumwa katika eneo hilo.

Benjamin amesema shughuli ya kuwapokonya silaha raia itaanza wakati wakatapopokuwa na maafisa wa polisi wa kutosha katika eneo hilo.

Mapigano makali yalizuka katika eneo hilo mwezi Agosti mwaka uliopita wakati watu wa kabila la Murle waliposhambulia kijiji kimoja na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 600 wa kabila la Lou Nuer.

Kufuatia mauaji hayo, watu wa kabila hilo la Lou Nuer waliunda jeshi lao ili kulipiza kisasi.

Tangu wakati huo mashambulio ya mara kwa mara ya kulipiza kisasi kati ya makabila hayo mawili yamekuwa yakitokea.