Wafungwa washona midomo Kyrgstan

Zaidi ya mahabusu elfu moja nchini Kyrgyzstan wamefunga midomo yao kwa kutumia uzi ili kulalamika kuhusu mazingira wanamoishi. Mamiya ya wafungwa hao walianza mgomo wa chakula wiki iliyopita kufuatia maandamano ndani ya gereza moja ambamo mtu mmoja aliuawa. Mwandishi wa BBC Rayhan Demytrie ana maelezo zaidi.

Maofisawa Kyrgyz wanasema kua wafungwa wapatao 1300 wameshona midomo yao na wengine takriban mia saba wanaendelea na mgomo wa chakula.

Wafungwa hao walichukua hatua ya kuziba midomo yao baada ya wakuu wa magereza kuwalazimisha kula. Mgomo huu ulianza kwa sababu wafungwa walitaka kumulika hali yao gerezani ambako mateso na kuwanajisi kumefanyika bila taarifa kutoka.

Wakuu wanadai malalamiko haya yamechagizwa na viongozi wa magenge ya wahalifu wanaopinga sheria mpya na kali ndani ya magereza.

Hata hivyo msemaji wa mojapo ya mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Kyrgyzstan aliyetembelea gereza anasema kua mojapo ya madai ya wafungwa hao ni kukomesha mateso.

Migomo ya chakula na maandamano ndani ya magereza ya Kyrgystan hutokea mara kwa mara, hususan kuhusu hali duni ndani ya gereza.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa aliyezuru nchi hio mwezi uliopita amesema kua hali katika baadhi ya magereza ni mbaya mno na tabia ya kuwanyanyasa wafungwa ni jambo la kawaida,